Maafisa wa polisi wa Kenya wakimpiga kwa mijeledi na marungu mwandamanaji wakati wa makabiliano katikati mwa jiji la Nairobi Juni 25, 2025
Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa (OHCHR) imeelezea wasiwasi wake kuhusu maandamano ya siku ya Saba Saba nchini Kenya, ambapo makumi ya raia wameuawa na wengine kujeruhiwa.
Katika taarifa yake siku ya Jumanne, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Türk alilaani ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Kenya, na kuahidi kutoa msaada kwa Kenya katika kutatua changamoto na katika uchunguzi.
"Tumesikitishwa sana na mauaji ya jana ya takriban watu 10, pamoja na uporaji na uharibifu wa mali nchini Kenya wakati polisi na vikosi vingine vya usalama vikijibu maandamano yenye ghasia katika mji mkuu wa Nairobi na kaunti zingine 16. Risasi za moto, risasi za mpira, gesi ya kutoa machozi na maji ya kuwasha vilitumika," ilisema OHCHR kupitia msemaji wake Shamsani Rada.
Türk ametoa wito wa utulivu, kujizuia, na kuheshimu uhuru wa kujieleza, kujumuika na kukusanyika kwa amani.
"Ni muhimu malalamiko halali ambayo ni mzizi wa maandamano haya yashughulikiwe," alisema.
Kamishna Mkuu pia alihimiza mauaji na ukiukwaji wote wa haki za binadamu "kuchunguzwa haraka, kikamilifu, kwa uhuru na kwa uwazi."
Wakati wa maandamano ya Julai 7, 2025, polisi waliripoti kwamba raia 11 waliuawa na 567 walikamatwa. Pia, Jeshi la Polisi (NPS) lilisema maafisa 52 na raia 11 walijeruhiwa, magari 12 ya polisi, magari 3 ya serikali na magari 4 ya raia yameharibiwa.
Maandamano yaliyoshuhudiwa siku ya Saba Saba yalikuja baada ya wiki mbili tu baada ya raia 15 kuuawa Juni 25, Wakenya walipoandamana kukumbuka mauaji ya zaidi ya watu 60 wakati wa maandamano yaliyoenea ya kupinga ushuru Juni 2024.
0 Comments