Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.
UJENZI wa Daraja la Mto Itembe lililopo wilayani Meatu Mkoani Simiyu, ambalo linagharamu kiasi cha Shilingi Bil. 8.4, unatarajia kukamilika Septemba 30, mwaka huu na litarahisisha Usafiri na Usafirishaji pia litafungua fursa za kiuchumi na kuongeza vipato vya wananchi.
Aidha, Kukamilika ujenzi wa daraja hilo kutaondoa adha ya watu kusombwa na Maji pia kufungua fursa za mawasiliano baina ya mikoa ya Arusha, Singida, Manyara na mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kukagua ujenzi wa daraja hilo, Msimamizi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Raphael Chasama, amesema kuwa ujenzi wa daraja hilo muhimu utaondoa kero zilizokuwa zinawakumba wananchi na umefiki
Amesema kuwa daraja hilo ni kiungo muhimu cha usafiri katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kaskazini huku akimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa miradi ya Maendeleo ikiwemo Barabara.
Ameongeza kuwa daraja hilo litarahisisha Usafiri na Usafirishaji wa mazao ya chakula na biashara na kwamba litachochea ukuaji wa Uchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mhandisi Emmanuel Kisanga kutoka kampuni ya Rocktronic Ltd amesema wanatekeleza Mradi wa ujenzi wa daraja la mto Itembe kwa gharama ya shilingi Bil. 8.4 ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 85.
"Tunatarajia kukamilisha ujenzi huu mwishoni mwa mwezi Septemba 2025 ili wananchi waanze kulitumia na kuondoa adha iliyokuwa inawakabili, tunamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi huu...pia tunawashukuru TANROADS Mkoa wa Simiyu kwa Usimamizi mzuri pamoja na kutuongezea ujuzi uliofanikisha ujenzi huu" amesema Mhandisi Kisanga.
Seif Abdalah, dereva wa lori na mkazi wa Mkalama mkoani Singida ameishukuru serikali kwa kutoa fedha za kujenga daraja hilo ambalo awali lilikuwa kikwazo cha usafiri na usafirishaji.
Naye Mabula Gukuba amempongeza hatua ya Ujenzi huo na kueleza kuwa miaka ya nyuma wananchi walikuwa wanapoteza maisha kwa kusombwa na maji wakijaribu kuvuka mto huo nyakati za masika.
Daraja hilo lenye urefu wa mita 150 na upana mita 11, likikamilika litakuwa daraja kubwa la kwanza Mkoani Simiyu ambalo limejengwa na Wakandarasi Wazawa kutoka Kampuni ya Rocktronic LTD.
MWISHO.
0 Comments