Header Ads Widget

CPA MAKALLA AWATAKA WAGOMBEA UBUNGE ,UDIWANI KUWA WAVUMILIVU HADI JULAI 28 ,2025

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

KATIBU wa NEC, Itikadi,Uenezi  na Mafunzo Chama, CPA Amoss Makalla, amewataka wagombea wote wa nafasi za Ubunge na Udiwani kuwa wavumilivu  na watulivu kwani kikao cha maamuzi kitafanyika Julai 28,2025 

Amesema kikao hicho ndicho kitatoa maamuzi ya mwisho kuhusu uteuzi wa wagombea watakaopitishwa na kuelekea hatua ya kura za maoni, kwa mujibu wa ratiba rasmi ya chama.

 “Wagombea wote wa ubunge na udiwani waendelee kuwa watulivu. Tunajua kuna hamasa na matarajio makubwa, lakini chama kinafanya kazi kwa umakini na kwa kuzingatia taratibu zote. Kikao cha maamuzi ni tarehe 28 Julai, na kutoka hapo tutaelekea kwenye kura za maoni,” alisema Makalla.

"Idadi ya wagombea ni kubwa, hivyo chama kinachukua muda kufanya uchambuzi wa kina ili kuhakikisha kila mmoja anatendewa haki kwa mujibu wa vigezo na kanuni,” aliongeza.

"Chama chetu ni makini,hatufanyi kazi kwa pupa tunataka kuhakikisha tunapata wagombea bora watakaoleta ushindi na maendeleo kwa wananchi,” alisema.

Amesema Mchakato huo wa uteuzi unaelekea katika hatua muhimu, ambapo wagombea waliopitishwa watachuana kwenye kura za maoni, kabla ya majina yao kuwasilishwa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi mkuu.

Aidha ameeleza kutakuwepo na  kikao cha Halmashauri kuu ya taifa 26 kitakachofanyika jijini Dodoma ambacho kitatanguliwa na kakao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa . 

CPA Makala pia alisisitiza kuwa chama kinasimamia mchakato huu kwa uwazi, umakini na haki, na kwamba hakuna mgombea atakayeachwa bila kuangaliwa kwa umakini.

Aidha, alieleza kuwa kikao hicho kitaanza kwa kikao cha Kamati Kuu, ambacho kitakuwa sehemu ya maandalizi ya mwisho kuelekea uteuzi rasmi, kabla ya kuanza kwa mchakato wa kampeni ndani ya chama.

Makalla amelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kuhairishwa kwa kikao ambacho kingefanya uteuzi tarehe 19 Julai Mwaka huu Jijini Dodoma. 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI