Na Matukio Daima Media
Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Dickson Mwipopo, amechangia kiasi cha shilingi milioni 2 kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCU) kilichopo mkoani Iringa, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuwaunga mkono vijana katika safari yao ya elimu ya juu.
Mwipopo alishindwa kufika moja kwa moja katika hafla hiyo, hivyo aliwakilishwa na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa, Dkt. Tumaini Msowoya.
Akizungumza kwa niaba ya Mwipopo, Dkt. Msowoya aliwakabidhi wanafunzi hao mchango huo na kusisitiza umuhimu wa nidhamu, maadili na uzalendo miongoni mwa vijana wanaosoma vyuo vikuu.
Katika hotuba yake, Dkt. Msowoya aliwataka wanafunzi wa mwaka wa kwanza kuwa makini na maisha ya chuo, akiwatahadharisha dhidi ya kujiingiza katika kile alichokiita “ndoa za rejareja”, pamoja na kujiunga na makundi yasiyo na mwelekeo mzuri.
Alisema kuwa baadhi ya wanafunzi hujikuta wakisahau lengo la msingi la kuja chuoni, ambalo ni kusoma na kujijenga kitaaluma, kutokana na kuathiriwa na mahusiano yasiyo rasmi.
“Najua mna miaka zaidi ya 18, hivyo kwa mujibu wa kawaida siyo watoto, lakini je, ndoa ndiyo imekuleta chuoni? Wazazi wenu wanajua mmeoa au mmeolewa mkiwa huku chuoni?” alihoji Dkt. Msowoya mbele ya wanafunzi, akisisitiza umuhimu wa uwazi na uwajibikaji kwa familia zao.
Aliongeza kuwa aliwahi kufanya utafiti kuhusu maisha ya wanafunzi wa vyuo vikuu na kubaini kuwa idadi kubwa yao huishi na wenza wao bila familia zao kufahamu jambo hilo. Kwa mujibu wake, hali hiyo ni hatari kwani huweza kuathiri masomo, afya ya akili na mustakabali wa wanafunzi hao.
Mbali na tahadhari hizo, Dkt. Msowoya aliwahimiza wanafunzi kuwa wazalendo wa kweli kwa kuipenda nchi yao, kuheshimu sheria na taratibu za chuo, pamoja na kujituma katika masomo yao. Alisema kuwa taifa linahitaji wasomi wenye maadili mema, uzalendo na uwezo wa kulisaidia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi, baadhi yao walimshukuru Dickson Mwipopo kwa mchango wake, wakisema fedha hizo zitawasaidia katika mahitaji mbalimbali ya kitaaluma na kuboresha mazingira yao ya kujifunzia. Waliahidi kuzingatia ushauri walioupata na kujitahidi kufikia malengo yao ya kielimu.
Mchango huo umeonekana kuwa faraja kubwa kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza RUCU, huku ukionyesha ushirikiano mzuri kati ya viongozi wa kisiasa na taasisi za elimu katika kuwawezesha vijana kufikia ndoto zao.


.jpg)




0 Comments