Header Ads Widget

OFISI YA CAG YAWANOA WAHABARI IRINGA...

NA BERDINA MAJINGE,MATUKIO DAIMA MEDIA IRINGA.

Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) imeendesha mafunzo maalum kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Iringa, kwa lengo la kuwaongezea uelewa katika kuandika masuala ya Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ( CAG)

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkaguzi Mkuu wa nje wa mkoa wa Iringa, CEA Lenatusi Leonard, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, katika kuimarisha uwazi na uwajibikaji kupitia Vyombo vya Habari.

CEA Leonard amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwapa uelewa zaidi wana habari ili waweze kuripoti kwa ufanisi habari za ofisi ya mkaguzi.

"Watumishi wa ofisi ya mkaguzi watatoa mada mbalimbali kwa ajili ya kuwajengea uelewa na uwezo wanahabari ili kuwaelimisha wadau wote ili wananchi waweze kupata taarifa sahihi za ukaguzi"amesema 

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano serikalini ofisi ya CAG Focus Mauki amesema kuwa kutokana na umuhimu wa vyombo vya Habari katika kuhabarisha umma CAG wameona ni muhimu kwanza kuwajengea uwezo wanahabari juu ya ukaguzi wa ufanisi.

Aidha amesema mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha waandishi wa habari kuelewa kwa kina aina mbalimbali za Ukaguzi, na namna ya kusoma na kuripoti taarifa za CAG, pamoja na mchango wao katika kuifikia jamii kwa taarifa sahihi.

"Vyombo vya habari vikijengewa uwezo, na hamana na kuona kwamba zile ripoti ni maudhui ambayo waandishi wanaweza kuyatumia kuandika kuhusu habari fulani wakiwa na takwimu sahihi"amesema Mauki

Amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa mwandishi wa habari kuzijua sheria na kuzitekeleza hasa katika uwajibikaji wa majukumu ya uandishi kwa kuzingatia taaluma.

"Ripoti za CAG zinapaswa kutangazwa hasa zile ambazo zinatangazwa kwa kuwa wananchi wengine hawana uwezo wa kufikia mtandao, lakini kupitia chombo cha habari wengi watafikiwa na kuelewa nini maana ya ripoti za ukaguzi za CAG"alisema

Mwenyekiti Iringa Press Club Frank Leonard amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia waandishi wa habari na wanawajibu wa kuwaeleza wananchi mapungufu yanayojitokeza ili mamlaka husika ziweze kushughulikia mapungufu hayo.

"Wanahabari wengi wamekuwa na hofu ya kuripoti habari zinazoleta changamoto kwa kuhofia wanaweza kujiingiza katika matatizo,"

"Wito wangu kwa wanahabari ni kuhakikisha wanaisaidia nchi kwa kuendelea kuifahamisha nchi yale yanayoibuliwa na ofisi ya CAG, kwa kufanya hivyo tunaamini mamlaka zingine zikiwemo TAKUKURU,Polisi wataweza kuingilia kati na kuchukua hatua zinazoweza kuzuia mambo yanayofanana na hayo yasiweze kujirudia"alisema Frank

Tukuswiga Mwaisumbe, ni miongoni mwa waandishi wa habari waliohudhuria mafunzo hayo amesema kuwa waandishi wengi wamekuwa na changamoto ya kupata ufafanuzi juu ya matumizi ya fedha za serikali kutoka katika mamlaka husika.

"Katika kutekeleza majukumu yetu tumekuwa tukipita katika miradi mbalimbali na kuona takwimu zinazotolewa haziendani na mradi wakti mwingine kuuliza inakuwa ni changamoto, hivyo kupitia mafunzo haya tumepewa namna ya kuingia katika wovuti na kuangalia taarifa au kuripoti muhusika ambaye amefanya ubadhirifu"alisema 

Mafunzo hayo ya ukaguzi kwa wanahabari yanatarajiwa kuongeza ufanisi wa Wanahabari wa Mkoa wa Iringa, katika kuripoti taarifa za Ukaguzi, jambo ambalo litasaidia kuimarisha uwazi, uwajibikaji na utawala bora nchini.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI