Header Ads Widget

BALOZI MAPURI AWAPA SOMO WATENDAJI WA UCHAGUZI KUTOKA DAR NA PWANI

 


Na Fatma Ally Matukio Daima Media

Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Balozi Omar Ramadhan Mapuri, amesema ili kuepuka malalamiko au vurugu zinazoweza kutokea wakati wa mchakato wa uchaguzi, ni muhimu kwa watendaji wote kufuata hatua za kikatiba na kisheria zilizowekwa.


Kauli hiyo ameitoa jijini Dar es Salaam wakati alipokua akifungua mafunzo ya siku tatu kwa mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi kutoka Mkoa ya Dar es Salaam na Pwani ambapo yamelenga kuwajengea uwezo watendaji hao kuweza kusimamia majukumu yao kwa weledi.


Amesema kuwa, kuna umuhimu wa kufuatwa kwa taratibu na hatua mbalimbali za kikatiba na kisheria zilizowekwa ili kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unakuwa wa haki, amani na usalama.


"Mafunzo haya yanahusisha waratibu wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo, maafisa wa uchaguzi pamoja na maafisa wa ununuzi, na yanatarajiwa kuendelea hadi Julai 23, 2025"amesema Balozi Mapuri.


Aidha, Balozi Mapuri alisisitiza kuwa, mafunzo hayo ni muhimu kwa kuhakikisha kuwa watendaji wa uchaguzi wanakuwa na uelewa mzuri wa majukumu yao na kwamba watashirikiana ipasavyo katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa usawa na haki.


"Mchakato wa uchaguzi ni jumuia ya jamii nzima na hivyo ni muhimu kwa kila mmoja wetu kuzingatia sheria na taratibu ili kuepuka migogoro yoyote inayoweza kujitokeza, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ina jukumu la kuhakikisha kuwa kila uchaguzi unafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia haki za kila mpiga kura" amesema Balozi Mapuri.


Hata hivyo, Balozi Mapuri amewataka watendaji wa  uchaguzi kuwa, ni muhimu kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu mchakato wa uchaguzi na kwamba watendaji hao watachukua hatua za haraka endapo kutatokea changamoto yoyote ili kuepusha madhara zaidi.


Sambamba na hilo, amesema kuwa ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha uchaguzi wa haki unafanyika bila kuvuruga utulivu wa taifa, kwani mchakato mzuri wa uchaguzi unahakikisha kwamba sauti ya kila raia inasikika na inaheshimiwa.


Ameongeza"Mafunzo haya yana lengo la kuboresha ufanisi wa uchaguzi katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, huku wakitarajia kupata wataalamu watakaowezesha mchakato wa uchaguzi kuwa na ufanisi na usalama wa hali ya juu"amesema Balozi Mapuri.


Mafunzo kama hayo yanafanyika kwa wakati mmoja katika mikoa mingine ya Shinyanga, Mwanza, Rukwa, Mbeya, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba, ambapo watendaji wa uchaguzi wa mikoa hiyo pia wanapata mafunzo ya namna bora ya kusimamia uchaguzi na kuzingatia taratibu za kisheria.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI