NA MATUKIO DAIMA MEDIA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, ametoa wito kwa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kuhakikisha kinakuwa na utendaji bora utakaochochea ushirikiano madhubuti kati ya Serikali na waajiri nchini.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa ATE uliofanyika jijini Dar es Salaam, Waziri Ridhiwani ameelezea umuhimu wa ATE katika kusimamia kwa umakini masuala ya wanachama wake kwa kuhakikisha waajiri wote wanazingatia kikamilifu Sheria za Kazi, hasa katika kuwapatia wafanyakazi mikataba halali ya kazi, pamoja na kuandaa mazingira bora ya kufanyia kazi ili kuongeza ustawi na tija kazini.
“Ni rai yangu kwa chama cha ATE kuendelea kuwa watendaji bora na kuhakikisha kuwa daraja bora la kuwaunganisha serikali na waajiri linaendelea kuimarika kwa kiasi kikubwa na niwaombe muendelee kusimamia kikamilifu masuala ya wafanyakazi ili kuhakikisha kuwa hakuna muajiri anayeshindwa kutekeleza sheria za kazi hususan katika kuwapatia mikataba ya kazi ambayo ni halisi lakini pia kuhakikisha uzingatiaji wa sheria unatekelezwa ipasavyo.
Mkutano huo uliambatana na uwasilishaji wa taarifa za kiutendaji kwa mwaka pamoja na kongamano maalum lililojadili mabadiliko ya sheria za kazi na athari zake kwa waajiri na waajiriwa.
Aidha ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuthamini ushirikiano wa Utatu wa Kazi unaowahusisha Serikali, Waajiri na Wafanyakazi, akisisitiza kuwa mabadiliko ya sheria yanalenga kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha Tanzania inasimamia vema mikataba ya kimataifa inayohusu haki za wafanyakazi.
Pia alitumia nafasi hiyo kulishukuru Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha utekelezaji wa mabadiliko hayo unaendana na viwango vya kimataifa vya kazi pia ametoa salamu za pongezi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa ILO Cde. Gilbert F.Houngbo
0 Comments