NA HABARI NA MATUKIO APP
WAJUMBE wa vikao vinavyopigania kura za maoni kwa wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametibuana kwenye mkutano wa jimbo la Kinondoni uliofanyika jana katika ukumbi wa Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo ulioitishwa na Mbunge wa Kinondoni, Abas Tarimba na kuhudhuria na wajumbe wa vikao vinavyopiga kura za maoni zaidi ya 6000, uliibua sintofahamu baada ya wajumbe kutofautiana kwenye mzozo wa nauli.
Mgeni rasmi katika mkutano huo alikuwa Katibu Halmashauri Mkuu (NEC), Oganaizasheni na Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Issa Gavu ambaye aliongozana baadhi ya viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam na wilaya ya Kinondoni.
Wakati mkutano huo ulioibua maswali ukiishia kwa sintofahamu miongoni mwao, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi amepiga marufuku ziara, mikutano, semina na makongamano ya aina hiyo, yanayohusisha wajumbe wa vikao vinavyopigania kura za maoni kwa wagombea wa ngazi zote.
Taarifa ya Dk. Nchimbi ambayo ilitoka saa chache baada ya mkutano huo wa Mbunge wa Kinondoni, ilisema kuwa marufuku hiyo inaanza mara moja mpaka baada ya kura za maoni kumalizika.
Dk. Nchimbi alisisitiza kuwa mwanachamna yeyote anayetarajia kugombea au wakala wake, analazimika kuepuka kufanya vitendo vyovyote vinavyoonekana dhahiri kuwa ni kinyume cha katiba, kanuni na miongozo ya chama chetu
Kuhusu mkutano huo uliomalizika kwa kurushiana kauli za vijembe miongoni mwa wajumbe, kulitokea baada ya mgeni rasmi na wengine kuondoka katika eneo hilo na kumwacha Mbunge akiendelea kuzungumza na wajumbe hao wa vikao vya maamuzi.
Tarimba ambaye tangaza kutetea kiti chake, aliitisha mkutano huo kwa lengo la kueleza utekelezaji wa Ilani ya CCM na kutangaza mafaniko aliyopata katika ujenzi miundombinu na miradi mbalimbali kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Dalili za kuwapo sintofahamu zilijionyesha tangu mwanzo wa mkutano huo kwani baadhi ya wajumbe waliohoji uhalali wa mkutano huo katika kipindi hiki cha lala salama na kwanini haukuhusisha wanachama wote wa CCM jimbo la Kinondoni.
“Kama huu ni mkutano wa wanaCCM wote kwa ajili ya kueleza utekelezaji wa Ilani ya chama, kwanini wameitwa wapigakura tu,?” alihoji mmoja wa wajumbe wa mkutano huo.
Mwandishi wa Raia Mwema ambaye alikuwapo eneo la mkutano huo, alishuhudia mzozo huo ambao uliibuka jioni baada ya wapambe wa Mbunge huyo kutoa nauli kwa kubagua.
Wapo wajumbe waliolipwa nauli ya sh 30,000 na wengine walikosa kabisa kwa sababu zilizoelezwa kuwa hawamuungi mkono Tarimba.
“Mkutano ulienda vizuri, viongozi walifungua na kondoka, kilichotokea ni kwamba baadhi ya wajumbe waliokuwa na mlengo tofauti na Tarimba, walinyimwa nauli, hapo ndo shughuli ilipoanzia,” alisema mjumbe mwingine wa CCM ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Kutokana na mzozo huo baadhi ya wajumbe waliotengwa waliibua mabango yenye ujumbe hasi kwa mbunge Tarimba.
Jimbo la Kinondoni ni moja ya majimbo ya moto kutokana na kuwepo makada maarufu wa CCM wanaotajwa kutaka kuwania kiti hicho kinachoshikiliwa na Tarimba.
Kabla ya mabadiliko ya Katiba ya CCM yaliyofanyika mwanzoni mwa mwaka huu, jimbo la Kinondoni lilikuwa na wajumbe maalum wa kura za maoni 400, lakini baada ya chama hicho kupanua wigo wajumbe wa kufanya mamuzi, jimbo hilo sasa lina wajumbe 6000.
0 Comments