Header Ads Widget

WAKULIMA ILULA KUNUFAIKA NA KILIMO CHA ALIZETI.

 


Na Berdina Majinge,

Matukio Daima.

KILOLO.Wakulima katika kitongoji cha Ikokoto, mji mdogo wa Ilula katika wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa wameshauriwa kuchangamkia fursa ya kilimo cha alizeti na kuacha kutegemea zao la nyanya peke yake kutokana na soko la zao hilo.

Ushauri huo umetolewa leo June 20, 2025 na Bwana shamba na mratibu wa kilimo Mkoa wa Iringa kutoka kampuni ya One Acre Tanzania Limited Emmanuel Kapela wakati wakitembelea shamba darasa lililopo kitongoji cha Ikokoto.

Kapela ameeleza kuwa lengo la kuanzisha shamba darasa ni kuhakikisha wanawafundisha wakulima kwa vitendo zaidi,ili elimu wanayoipata wakaitekeleze katika mashamba yao binafsi.

"Tunatarajia mkulima akilitunza shamba lake vizuri kwa kufuata njia bora za kilimo, tunauhakika atavuna gunia 13-23 kwa maana ya kilo 800 hadi 1400 za Alizeti"alisema


kapela alieleza kuwa mkulima anayelima alizeti na mahindi kwa pamoja. zao la mahindi linamsaidia anakuwa na usalama wa chakula nyumbani kwake, na alizeti akishavuna anauwezo wa kuiuza kama ilivyo au kukamua mafuta ambayo kwa gunia moja anauwezo wa kupata lita 24 za mafuta.

"Malengo kwa msimu ujao ni kuhakikisha wanaongeza wigo zaidi wa kuanzisha mashamba darasa mengi zaidi kwa mkoa wa Iringa, ambapo mradi wa One Acre Tanzania Limited umefika kuhakikisha inaleta tija kwa wakulima"

mradi huo wa kilimo cha alizeti ulianza mwaka jana ambapo kwa kushirikiana na wizara ya kilimo walisambaza mbegu za alizeti bila gharama yeyote kwa wakulima kuhakikisha tunaongeza chachu kwa wakulima na kutambua zao la alizeti lina tija.


Ameeleza kuwa wakulima zaidi ya 130,000 Mkoani Iringa wamepewa pembejeo na  mafunzo na kampuni ya one Acre Tanzania Limited 

kampuni inawahakikishia wakulima kupata pembejeo zenye ubora na kutoa mafunzo kitaalamu ili kuwafanya wakulima kulima kitaalamu zaidi.

one acre Tanzania Limited inawawezesha na kuwahimiza wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kupanda miti ili kurejesha uoto wa asili ili mabadiliko ya tabia nchi yasije kuwa na madhara makubwa kwa wakulima.

Akizungumza mmoja wa wakulima hao Destar Magubike ameeleza kuwa mafunzo hayo kupitia shamba darasa limewasaidia kwa sababu kilimo walichokuwa wanalima cha alizeti walikuwa hawapati mavuno mazuri ili kukidhi mahitaji yao 

"Hizi alizeti za kisasa zinatusaidia kwa sababu ni mbengu ambayo inavumilia ukame na ukilima inasitawi, namna ya utunzaji wako na ukipalilia kuweka mbolea na inastamili sana pia inatuwezesha kupata mafuta bora ya kupikia"


Naye Samwel Jeremia Mkulima kutoka Kijiji cha Ikokoto, anasema kuwa alizeti ni kilomo bora ambacho hakitumii gharama kubwa na hakisumbui kama mazao mengine na wamependezwa na mbegu hiyo.

 Rachel Mahinya mkulima kutoka kikundi cha Agape alisema kutokana na  elimu duni ya uzalishaji wa alizeti na upatikanaji wa pembejeo unakuwa haupo kwa watu wenye kipato cha chini ndio sababu ya wao kushindwa kufikia lengo.


"Kupitia elimu hii tuliyopewa nimejifunza kuwa kupitia eneo dogo naweza kupangilia zao langu la alizeti na kulima kilimo cha kisasa na chenye tija hasa katika uzalishaji wa mafuta ya alizeti,kwa sasa kilimo cha nyanya hakieleweki hivyo tunapaswa kuangalia fursa zingine kama kilimo cha alizeti ili wananchi wawe na uhakika wa kipato"alisema

"Ilula wakulima wengi walijikita na kilimo cha nyanya ambacho wakati mwingine hakieleweki watu wanapata na kukosa na wakulima wengi walipotea kutokana na elimu duni na kusahau kuwa kilimo cha alizeti kinaweza kuwapatia mapato mazuri ya kukidhi familia"

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI