Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe amekabidhi zawadi za pikipiki kwa wakulima hodari kutoka Amcos ya Itemelo iliyoko Kata ya Dutwa wilayani Bariadi Mkoani Simiyu baada ya kuzalisha Pamba kwa kuzingatia ubora na tija.
Zawadi hizo zimetolewa ikiwa ni ahadi ya Waziri huyo aliyoitoa mara baada ya kutembelea Amcos hiyo katika msimu wa kilimo 2023/24 na kuahidi kuwa endapo watafikisha uzalishaji wa kilo 1000 kwa ekari, atawakabidhi zawadi.
Akikabidhi juzi kwa niaba ya Waziri Bashe, Mkaguzi wa Pamba wilaya ya Bariadi kutoka Bodi ya Pamba, Anthoy Ndinda amesema kuwa zawadi hizo zimetolewa ikiwa ni sehemu ya motisha ili kutimiza ahadi iliyotolewa na Waziri kwa wakulima hao.
Amesema kuwa wakulima hao wamepewa zawadi hizo kutokana na kuzalisha Pamba bora na kwa tija zaidi ya kilo 1000 kwenye ekari moja.
"Nawaasa wakulima wa pamba, wafuate kanuni na Utaalamu wanaopewa na Maafisa Kilimo...pongezi nyingi ziende kwa Waziri wa Kilimo (Bashe) muasisi wa Mpango wa Jenga Kesho Bora (BBT), wilaya ya Bariadi tuna Maafisa Ugani wa BBT zaidi ya 80 ambao wamehudumia wakulima na wakafuata utaalamu na maelekezo" amesema.
Anasema kuwa wakulima hao walizingatia kanuni za kilimo cha Pamba ikiwemo matumizi ya mbolea hai, kupanda kwa nafasi na kwamba wakulima wa Kata ya Dutwa walinufaika na ruzuku ya mbolea hai za Serikali.
Katika hatua nyingine, Ndinda anasema wilaya ya Bariadi wanatarajia kuzalisha kilo Mil. 36 kutokana na serikali kupeleka Pembejeo kwa wakati pamoja na huduma za Ugani kuwafikia wakulima kwa usahihi.
Joshua Matongo, mkulima kutoka Kijiji cha Igaganulwa anasema anampongeza Waziri Bashe kwa kutambua mchango wao katika sekta ya Pamba na kuwapatia zawadi ambazo zitaongeza motisha kwa wakulima hao.
Mwenyekiti wa Itemelo Amcos, Juliana Mayenga amesema amefarijika baada ya kuona ahadi ya Waziri wa Kilimo (Bashe) inatekelezwa kutokana na Wakulima hao kufuata kanuni za kilimo bora cha Pamba.
"Waziri Bashe alifikawaka ,2023 na kuahidi endapo watazalisha kilo 800 mpaka 1000 watapewa zawadi, le ametimiza kutoa ahadi tunamshukuru sana...Wakulima wajifunze kwa wakulima hawa ili kuongeza tija ya uzalishaji wa Pamba" amesema.
Mwisho.
0 Comments