Na Josea Sinkala.
Ndugu Geoffrey Mwankenja mkazi wa Chunya mjini mkoani Mbeya ametumia zaidi ya shilingi milioni mia tatu kwa ajili kuwezesha miundombinu ya umeme, maji na usafiri wa boti mto Lupa Kijiji cha Mbigwa Chokaa Wilayani Chunya.
Ni umbali wa zaidi ya kilometa thelathini kutoka Chunya Mjini ambako Geoffrey Mwankenja mdau wa maendeleo alikowekeza leseni ya kitalu cha uchimbaji madini ya dhahabu.
Katika uwekezaji wa miundombinu ya umeme Mwankenja ambaye anatajwa kuwa na dhamira ya kuwania ubunge Jimbo la Lupa (CCM), ametumia zaidi ya shilingi milioni mia mbili hamsini huku akitumia zaidi ya shilingi milioni sitini kwa ajili ya visima vitatu huku akitumia shilingi milioni kumi kwa ajili ya kuvusha watu na bidhaa kutoka Kata ya Matundasi na Kata ya Chokaa.
Mwankenja amerejea nchini akitokea nchini Marekani ambako alikuwa akifanya kazi katika mashirika mbalimbali hivyo ameamua kurejea nchini kutokana na fursa nyingi zilizopo na uboreshaji wa miundombinu hasa katika Serikali ya awamu ya tano na sita.
Mwankenja amesema katika visima vitatu alivyochimba visima viwili amevichimba kwa pesa zake na kimoja kimechimbwa na rafiki zake waliopo Marekani.
Aidha Mwankenja amemmwagia sifa Mhe. Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyoifungua nchi katika sekta mbalimbali zikiwemo za madini, kilimo na utalii hivyo kuiomba Serikali iendelee kuwekeza hususani barabara ya Makongolosi kwenda Tabora.
Alfonce Mkumbwa ni mkazi wa Makatang'ombe wilayani Chunya, amesema kuwepo kwa umeme katika eneo la machimbo kumerahisisha uchimbaji kwani awali walikuwa wakichimba kwa kutumia sululu hali iliyowalazimu kutumia gharama kubwa na wao kupata kipato kidogo.
Akizungumzia huduma ya maji Mkumbwa amesema visima hivyo vimepunguza maradhi ya tumbo kutokana na awali kutumia maji ya mto Lupa ambayo si salama.
Naye Agnes Mhagama Mama Ntilie amesema awali walikuwa wakitumia maji ya mto Lupa mbali ya kuhofia usalama wake walikuwa wakipoteza muda mwingi kwenda kuteka maji mto Lupa.
Baadhi ya vijana wanaofanya kazi katika kitalu cha uchimbaji madini ya dhahabu inayomilikiwa na Geoffrey Mwankenja wamesema kwa sasa hakuna sababu za kukaa mjini bila kazi kwani Serikali na wawekezaji wameboresha miundombinu inayowasaidia kujipatia kipato hivyo kuondoa tatizo la ukosefu wa ajira nchini.
Katika leseni ya kitalu cha uchimbaji madini ya dhahabu inayomilikiwa na Geoffrey Mwankenja ameweza kupata wawekezaji wa Kitanzania,Warusi, Washindi na Afrika Kusini ambapo kupitia utaalam na Teknolojia ya kisasa kumekuwa na ongezeko la upatikanaji wa dhahabu unaongeza maduhuri ya Serikali.
Akihitimisha Geoffrey Mwankenja amesema kiu yake ni kuwatumikia wananchi kupitia nafasi ya Ubunge Jimbo la Lupa kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) licha ya kura kutotosha vipindi viwili bado hajakata tamaa na anatamani kufanya makubwa zaidi endapo atapewa ridhaa na wajumbe pia wananchi wa Wilaya ya Chunya bila kujali itikadi zao.
Pia mdau huyo wa shughuli za maendeleo amekemea baadhi ya watu wanaoeneza chuki za ukanda na ukabila tabia ambayo anasema si njema na ilishakemewa na viongozi mbalimbali akiwemo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere badala yake wanaaswa kuimarisha upendo na umoja.
0 Comments