Na Hamida Ramadhan, Dodoma
TANZANIA imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kuongeza Uelewa kwa Watu Wenye Ualbino, kwa kufanya maadhimisho ya kitaifa mkoani Kigoma huku ikielezwa kuwa jitihada za kiuchumi kwa kundi hilo zinaendelea kuzaa matunda.
Wakati wa maadhimisho hayo, watu wenye ualbino walilipongeza Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) kwa kuendelea kuwawezesha kiuchumi kupitia miradi bunifu, ikiwemo uzalishaji wa mkaa mbadala.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali linaloshughulika na haki za watu wenye ulemavu, Foundation For Disabilities Hope (FDH), Bw. Maiko Salali, alisema kuwa msaada wa STAMICO umekuwa chachu ya mabadiliko kwa maisha ya watu wenye ualbino.
“Tunaishukuru sana STAMICO kwa kuendelea kusaidia watu wenye ualbino nchini. Mradi wa uzalishaji wa mkaa mbadala umewasaidia kuongeza kipato na pia kulinda afya zao dhidi ya athari za nishati chafu,” alisema Salali.
Maadhimisho ya mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu inayolenga kuhamasisha usawa, ulinzi na ujumuishwaji wa watu wenye ualbino katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Siku ya Kimataifa ya Kuongeza Uelewa kwa Watu Wenye Ualbino huadhimishwa kila mwaka tarehe 13 Juni, ikiwa na lengo la kuelimisha jamii kuhusu changamoto wanazokumbana nazo watu wenye ualbino, na kuhamasisha mapambano dhidi ya unyanyapaa, ubaguzi na ukatili.
Kwa miaka ya hivi karibuni, serikali na mashirika mbalimbali yamekuwa mstari wa mbele kuboresha hali ya maisha ya kundi hili kupitia fursa za elimu, ajira na miradi ya maendeleo, hasa maeneo ya vijijini ambako changamoto zao zimekuwa kuwa kubwa zaidi
0 Comments