Na Moses Ng’wat, Songwe.
Katika tukio lililojaa hisia na huzuni kubwa, aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Happiness Seneda, ameagana rasmi na watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, baada ya kuhudumu kwa kipindi cha miaka mitatu Mkoani humo.
Hafla hiyo ya kuagana imefanyika Juni 26, 2025 katika ukumbi mdogo wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ilihudhuriwa na watumishi mbalimbali waliojaa hisia za shukrani, wakimwelezea Seneda kama kiongozi aliyewaunganisha na kusimamia haki kwa vitendo.
Seneda, ambaye amehitimisha rasmi safari yake ya kikazi Mkoani Songwe, ameweka bayana nia yake ya kuingia kwenye siasa, akieleza mpango wa kugombea ubunge katika uchaguzi ujao.
Miongoni mwa watumishi waliomzungumza kwa niaba ya watumishi wengine, Katibu Tawala Msaidizi Rasilimali watu na Utawala , Wilfred Muyuyu, ameeleza kwa hisia jinsi Seneda alivyokuwa mfano wa uongozi makini na usio na ubaguzi.
"Kwa muda uliokuwa hapa umekuwa kiongozi mwenye utulivu mkubwa hata pale tulipopata mawimbi...nakumbuka idara nyingi zilikuwa na watendaji waliokaimu, lakini leo tunashuhudia kila idara imepta kiongozi wake na hayo yote ni matunda yako" amesema Muyuyu.
Aidha, watumishi wote waliopata nafasi ya kuzungumza kwenye hafla hiyo walimpongeza kiongozi huyo kwa ujasiri wa kuwasikiliza watumishi wote bila kujali nafasi zao na hali ambayo imeleta mabadiliko chanya katika mfumo wa kazi mkoani himo na kuongeza ari ya utendaji.
Kwa upande wake, Seneda alitumia fursa hiyo kuwashukuru watumishi wote kwa ushirikiano waliompa na kuwaasa kuendeleza mshikamano huo kwa Katibu Tawala mpya, Dkt. Frank Hawasi, ambaye ameteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Nawashukuru kwa ushirikiano, mapenzi na mshikamano, na mafanikio yote haya si yangu pekee, bali ni ya kila mmoja aliyeshiriki kujenga Songwe"
"Na naomba kuwaambia watumishi msiogope kuwekeza hasa kwa mkoa huu wa Songwe ambao una fursa nyingi".
Aidha, Seneda pia amewashukuru waandishi wa habari na vyombo vya habari Mkoani Singwe kwa namna walivyosaidia kuutangaza mkoa wa Songwe kwa habari chanya na za kuleta matumaini.
"Waandishi wamekuwa mabalozi wazuri wa mkoa wetu na naomba msiwachukulie kama kuwa maadui, bali hawa ni marafiki wa maendeleo ya mkoani hapa," alisisitiza.
Seneda pia alimpongeza aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, kwa ushirikiano waliokuwa nao na kumtakia kila la heri katika safari yake mpya ya kisiasa, akieleza kuwa nae ameonesha nia ya kugombea ubunge katika Jimbo la Makambako.
Wakati wa kuagana, watumishi wengi walionekana wakibubujikwa na machozi, ishara ya upendo wa dhati waliokuwa nao kwa kiongozi huyo ambaye amewaacha wakiwa na kumbukumbu ya uongozi wa kipekee uliotanguliza utu na mshikamano.
Mwisho.
0 Comments