Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima App Dodoma
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson,ameongoza hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Bunge ya Wavulana katika eneo la Kikombo jijini Dodoma.
Shule hiyo itakuwa ya mchepuo wa sayansi na inalenga kuendeleza elimu kwa watoto wa kiume kwa viwango vya juu na mazingira rafiki ya kujifunzia.
Akizungumza katika hafla hiyo, Spika Tulia amesema kuwa wazo la kuanzisha shule hizo lilianzia kwa wabunge wanawake waliokuwa na lengo la kushughulikia changamoto za watoto wa kike katika elimu.
"Baada ya mafanikio ya Shule ya Bunge ya Wasichana, sasa juhudi hizo zimepanuliwa kwa watoto wa kiume ili kuwe na usawa wa kijinsia katika fursa za elimu, " Amesema
Hata hivyo amesema , Bunge ni taasisi ya wananchi wote, hivyo ni wajibu wake kuhakikisha watoto wote wa kike na wa kiume wanapata mazingira bora ya kusoma na kufikia ndoto zao.
" Shule hiyo itajengwa kwa viwango vya kisasa na kuwa mfano wa kuigwa kwa ubora wa elimu na nidhamu," Amesema.
Ujenzi wa shule hiyo unakadiriwa kugharimu shilingi bilioni tatu ambapo fedha za awali zimepatikana kupitia michango ya wabunge kwa kutumia sehemu ya posho zao, ushiriki wa wabunge wa majimbo, mbio za hisani maarufu kama Bunge Marathon pamoja na misaada kutoka kwa taasisi za kifedha na makampuni binafsi bila kuwasahau wananchi.
Aidha Spika Tulia ametoa wito kwa wadau wengine kuendelea kuchangia ili kufanikisha ujenzi wa shule hiyo kwa wakati.
Amesema kuwa Bunge liko wazi kupokea michango ya aina yoyote kutoka kwa mtu mmoja mmoja, kampuni au taasisi, kwa kuwa mradi huo ni wa kizazi kijacho.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bunge Bonanza Festo Sanga amesema kwa niaba ya Kamati Tendaji amesema kuwa maono ya ujenzi wa shule hiyo yalitokana na wazo la Spika Tulia kupitia mazoezi ya pamoja ya wabunge.
Alisema awali Bonanza lilikuwa na lengo la kuimarisha afya na mshikamano wa wabunge lakini sasa limekuwa chimbuko la mradi mkubwa wa elimu kwa wavulana.
Ameeleza kuwa eneo lililotengwa kwa ajili ya shule hiyo ni kubwa, zuri na linalofaa kabisa kwa ujenzi wa shule ya kisasa itakayokuwa na maabara, mabweni, maktaba, madarasa ya kisasa pamoja na viwanja vya michezo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mayeka Mayeka amesema ujenzi wa shule hiyo ni jambo la kujivunia kwa mkoa huo.
Amesema mradi huo utaongeza thamani ya Dodoma kama makao makuu ya nchi na kuwa kitovu cha miradi mikubwa ya maendeleo ya elimu.
Mayeka ameongeza kuwa mradi huo unaendana na maono ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bora bila kujali jinsia, mahali walipo au hali yao ya kiuchumi.
Shule ya Bunge ya Wavulana itakuwa ni ya pili kuanzishwa chini ya mpango wa Bunge wa kuwekeza kwenye elimu ya watoto, baada ya ile ya wasichana ambayo tayari inatoa matokeo chanya kwa taifa.
Mwisho
0 Comments