Rwanda na DR Congo hazikusaini mkataba wa amani kama ilivyotarajiwa,kama ilivyotangazwa na waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Olivier Ndu-hu-ngire-he.
Mkataba huo, uliratibiwa na Marekani ili kukomesha mapigano mashariki mwa DRC, ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na wengine wengi kuyahama makazi yao.
Mwezi Aprili, Rwanda na Jamuhuri ya demokrasia ya Congo walikubaliana wakati wa mazungumzo na Washington kuandaa makubaliano ya amani yenye lengo la kumaliza mgogoro wa mashariki mwa DRC, huku utiaji saini huo ukipangwa kufanyika jana jumapili.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Rwanda Olivier Nduhungirehe alichapisha kwenye X kuwa "Hakuna makubaliano ya amani yatakayotiwa saini Jumapili hii tarehe 15 Juni 2025 huko Washington."
Waziri huyo alisema mchakato wa mazungumzo bado unaendelea na kwamba utiaji saini utafanyika mara tu "makubaliano ya amani yanayofaidi kila upande yatakapofikiwa na pande zote.
Nduhungirehe alionya wale wanaohusika na "kuvujisha kwa makusudi habari za upande mmoja" kwa vyombo vya habari, akisema "inaweza kuhatarisha" mazungumzo.
Haya yanajiri siku chache baada ya Rwanda kujiondoa katika jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika ya Kati, ikishutumu jumuiya hiyo kuegemea upande wa DRC.
0 Comments