NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
Katika juhudi za kuboresha upatikanaji wa huduma na kuhakikisha ufanisi kwa wanachama wake, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeongeza matumizi ya teknolojia ya kisasa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa njia ya mtandao.
Akizungumza katika warsha ya siku moja kwa waandishi wa habari jijini Mwanza tarehe 12 Juni 2025, Kaimu Meneja wa PSSSF Kanda ya Ziwa Mashariki, Happiness Manyenye, alisema kuwa wanachama wa mfuko sasa wanaweza kufanya shughuli mbalimbali kupitia mifumo ya kidijitali kama vile ‘PSSSF Portal’ na ‘PSSSF Kiganjani’.
“Teknolojia imerahisisha maisha ya wanachama wetu. Hawalazimiki tena kusafiri hadi ofisi zetu kwa ajili ya kujisajili, kuwasilisha madai au hata kuona michango yao. Kila kitu kinafanyika kupitia simu janja au kompyuta,” alisema.
Manyenye pia alieleza kuwa, licha ya mafanikio hayo, changamoto ya usalama wa taarifa imeibuka, ambapo baadhi ya wastaafu wamekuwa wakilengwa na matapeli wanaotuma ujumbe wa simu wakijifanya ni maafisa wa PSSSF.
“Tunaendelea kuelimisha wanachama wetu kuwa PSSSF haitumi ujumbe kutoka namba binafsi. Taarifa rasmi hutumwa kwa jina la taasisi, hivyo mtu yeyote anayepokea ujumbe wa aina hiyo anatakiwa kufika ofisini kuthibitisha,” alionya.
Kwa mujibu wa taarifa, baadhi ya wastaafu walipokea ujumbe uliojumuisha namba ya ‘check’ au madai ya malipo, hali iliyowatia hofu hadi walipofika ofisini kwa uhakiki.
Katika kuboresha zaidi huduma, PSSSF imeongeza kiwango cha chini cha pensheni kutoka shilingi 100,000 hadi 150,000 kwa mwezi, kuanzia Januari 2025. Aidha, mfuko umeanzisha fao la msaada wa mazishi kwa familia ya mstaafu aliyefariki dunia. Vilevile, pensheni itaendelea kulipwa kwa kipindi cha miezi 36 baada ya mstaafu kufariki, ambapo malipo hayo yataelekezwa kwa mke au watoto walio chini ya miaka 21.
Muuguzi mstaafu Jane Kalimasi kutoka Mwanza alisema huduma hizo za kidijitali zimeleta nafuu kubwa kwa wastaafu. “Sasa ninaweza kupata taarifa zangu kupitia simu bila usumbufu. PSSSF wamekuwa wakitukumbusha kwa ujumbe, jambo ambalo limetusaidia sana sisi wazee,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza, Edwin Soko, alihimiza wanahabari kuendelea kuelimisha jamii kuhusu huduma za hifadhi ya jamii, ili wananchi waweze kujua umuhimu wa kujiunga na mifuko hiyo kwa ajili ya usalama wa maisha yao ya baadaye.
0 Comments