Header Ads Widget

NAIBU WAZIRI SANGU AWATAHADHARISHA WAGOMBEA KUJIEPUSHA NA RUSHWA MAJIMBONI, TAKUKURU IPO KAZINI


Na Mwandishi Wetu- NZEGA 

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu amesema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imejidhatiti kuhakikisha inadhibiti vitendo vya rushwa kabla, wakati na hata baada ya Uchaguzi Mkuu huku akiwaasa wagombea kujiepusha na vitendo vya rushwa huko majimboni kwani TAKUKURU ipo kazini.

Amesema kitendo cha  Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kutoa jumla ya magari mapya  195 kwa ajili ya  TAKUKURU ni uthibitisho tosha kuwa anachukia vitendo vya rushwa.

Mhe.Sangu ametoa kauli hiyo leo  wakati akizindua Jengo la TAKUKURU  Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora ambalo limegharimu kiasi cha Sh. Mil. 314.2 hadi kukamilika kwake.


Amesema TAKUKURU  itawakamata wale wote watakaothubutu kutoa rushwa ya aina yeyote ile kwa lengo la kuwarubuni wapiga kura "Msikubali kurubuniwa na rushwa na atakayethubutu kufanya hivyo  toeni taarifa kwa TAKUKURU" amesisitiza Mhe.Sangu

Amesema mbali ya kutoa magari hayo, katika kipindi chake cha uongozi Rais.Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za kujenga jumla  ofisi  25 katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini kwa lengo la kuwawezesha watumishi wa TAKUKURU  kufanya kazi katika mazingira rafiki hususan katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu

Aidha, Mhe. Sangu amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa alioufanya kwa taasisi hiyo ambapo katika kipindi chake cha uongozi ameajiri watumishi wapya  1900 ikiwa ni nusu ya watumishi aliowakuta


Akizungumzia madhara ya kuchagua viongozi kwa njia ya rushwa, Mhe, Sangu amesema vitendo vya rushwa na makosa mengine yanayofanyika wakati wa uchaguzi huwapoka  wapiga kura haki ya kumchagua  mgombea wanayemtaka.

Ameongeza kuwa vitendo hivyo vya rushwa huwanyima haki baadhi ya wagombea kushiriki na kushindana kwa usawa katika uchaguzi.

Naye Mkuu wa wilaya ya Nzega, Mhe. Naitapwaki Tukai amesema yeye kama Mwakilishi wa Rais katika  wilaya hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya TAKUKURU wamejidhatiti kuhakikisha hakuna mtu yeyote atakayechaguliwa kuwa Kiongozi katika wilaya hiyo kwa njia ya rushwa.


" Mtu yeyote mwenye nia ya kugombea katika uchaguzi Mkuu kwa njia ya rushwa,   hana nafasi katika Wilaya hii amesisitiza Mhe. Tukai

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Chalamila amesema TAKUKURU imewezeshwa vitendea kazi hivyo jukumu walilonalo kwa sasa ni kufanya kazi kwa maslahi ya taifa kabla, baada na hata baada ya Uchaguzi Mkuu. 



 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI