Francisca Mustapha Ng'aumbwa (mwenye tisheti nyeupe)Nesi wa Macho wa taasisi ya CEVO akitoa elimu kwa watoto waliofika hospitali ya wilaya Mabwepande Dar es Salaam ilikofanyika kampeni ya utoaji elimu na upimaji wa macho bure kwa udhamini wa taasisi hiyo.
NA ARODIA PETER
KENGEZA, ni hali ambayo macho yote mawili hayawezi kuzingatia mwelekeo mmoja kwa wakati mmoja.
Wakati jicho moja linaweza kuzingatia kitu kinachozingatiwa, jicho la pili linaweza kugeuka ndani, nje, juu, au chini kwa wakati mmoja.
Ingawa wataalam wanasema kengeza linatibika, jamii nyingi za kiafrika hawana taarifa za kutosha juu ya tiba hiyo na wamekuwa wakiona ni ulemavu wa kawaida.
Hata hivyo wataalam wa tiba wanabainisha kuwa mtu aliyezaliwa na macho yenye kengeza anaweza kupata tiba na kupona kabisa endapo atawahi matibabu.
Akizungumza kwenye kampeni maalum ya uhamasishaji na upimaji wa macho bure katika hospitali ya wilaya Mabwepande mkoani Dar es Salaam kwa siku mbili mfululizo, Juni 12, 13, 2025, Mkurugenzi na mwanzilishi wa Taasisi ya Child Eye and Vision Organization, Dkt Asha Mweke alisema mtoto mwenye jicho la kengeza kuanzia miaka 2 hadi 18 anatibika kwa urahisi zaidi.
Alisema mwenye umri huo akiwahi matibabu anaweza kutibika kwa kuvaa miwani maalum na kupona kabisa.
Dkt Asha alisema kampeni yao ina lenga kuibua watoto wenye changamoto ya afya ya macho ili waweze kupata tiba mapema kwa sababu baadhi ya changamoto zisipodhibitiwa kwa wakati zinasababisa uoni hafifu na hata ulemavu wa kudumu.
“Kuna aina mbalimbali ya magonjwa ya macho, kwa mfano mtoto aliyezaliwa na mtoto wa jicho, kansa ya macho au mboni nyeupe, asipotibiwa mapema anaweza kupata ulemavu wa kudumu na hata kifo.
“Taasisi yetu imejikita katika kuwaibua watoto wenye changamoto hizo na kutoa elimu kupitia mikutano ya wazazi shuleni kwa kutoa elimu kwa wazazi, walezi na walimu ili waweze kuwabaini mapema na kupatiwa matibabu sahihi”alisema Dkt Asha na kuongeza kuwa
“Kupitia kauli mbinu ya mwaka huu inayosema ‘Mboni ya mwanangu, wajibu wangu’ tunataka kutengeneza kizazi cha watu wanaoona vizuri Tanzania, Afrika na duniani kwa ujumla.
Huu ni mwaka wa tatu mfululizo, CEVO inaadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika kwa kuhamasisha elimu juu ya umuhimu wa afya ya macho kwa watoto na watu wengine kwa ujumla.
Dalili ambayo inaweza kukusaidia kutambua ikiwa mtu anaugua jicho la makengeza ni pamoja na macho hutembea kwa kujitegemea kutoka kwa kila moja, matokeo yake macho yote hawezi kuangalia kwenye doa moja kwa wakati mmoja.
Inaweza pia kutokea kwa sababu ugonjwa wa ubongo una maana kuwa macho hayawezi kuratibu usahihi.
Mwisho
0 Comments