Na Ashrack Miraji Matukio Daima
Lushoto, Tanga – Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2025 ukiwa katika ziara yake ya kitaifa Nwishoni mwa wiki hii , ulitua katika Wilaya ya Lushoto na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.8. Mwenge huo ukiwa unaongozwa na Mkimbiza Mwenge wa Kitaifa, Ndugu Ismail All Ussi, ulipokelewa kwa shamrashamra kubwa na wananchi wa Lushoto wakiongozwa na viongozi wa Serikali, wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama, na viongozi wa dini.
Katika ziara hiyo, miradi iliyokaguliwa ilihusisha sekta za afya, elimu, maji na barabara. Mkimbiza Mwenge alipongeza utekelezaji mzuri wa miradi hiyo na kuhimiza wananchi kuitunza kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. Aidha, alisisitiza kuwa miradi hiyo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya uongozi wa halmashauri na viongozi wa kisiasa katika wilaya hiyo.
Akizungumza wakati wa mkesha wa Mwenge uliofanyika katika viwanja vya Lushoto mjini, Ndugu Ismail All Ussi alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Lushoto, Mheshimiwa Shaban Shekilindi, kwa kazi kubwa anayofanya ndani ya jimbo hilo. Alisema mbunge huyo ameonesha uzalendo wa kweli kwa kushirikiana kwa karibu na ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Lushoto katika kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inasimamiwa kikamilifu.
"Ndugu zangu wa Lushoto, mna bahati kubwa kuwa na kiongozi mwenye maono kama Mheshimiwa Shekilindi. Ameendelea kuiwakilisha vyema Lushoto bungeni na kuhakikisha mnapata mgao mkubwa wa rasilimali kutoka Serikali Kuu," alisema Ussi mbele ya umati wa wananchi.
Katika hotuba yake, Mbunge Shekilindi naye hakusita kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuipatia Lushoto fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Alisema kuwa Rais Samia ameendelea kuwa kielelezo cha kiongozi anayejali wananchi wake, na kwamba wananchi wa Lushoto hawana deni lingine kwake isipokuwa kumpigia kura ya kishindo ifikapo Oktoba 2025.
"Rais wetu mpendwa ametuamini, ametuletea fedha nyingi za miradi, jukumu letu sasa ni kuhakikisha tunamuunga mkono kwa vitendo. Sisi kama viongozi wa Jimbo tumejipanga kuhakikisha kila fedha inayokuja inaleta tija kwa wananchi," alisema Shekilindi kwa msisitizo.
Aidha, Mbunge huyo alitoa wito kwa wananchi wa Lushoto kuendelea kuimarisha mshikamano na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, akisema kuwa maendeleo hayataletwa na mtu mmoja bali nguvu ya pamoja ya jamii nzima.
Mkimbiza Mwenge wa Kitaifa aliwataka vijana wa Lushoto kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani, matumizi ya dawa za kulevya na kushiriki kikamilifu Katika uchanguzi Mkuu na kulinda amani ya Taifa letu, akisema kwamba maendeleo hayapatikani bila utulivu na mshikamano wa kitaifa.
0 Comments