Header Ads Widget

MIRADI YA KIJAMII YAPUNGUZA UJANGILI SERENGETI

 


Ofisa Mahusiano ya Jamii wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Abed Mwesigwa akionyesha moja ya madaraja yaliyojengwa na hifadhi hiyo wilayani Serengeti mkoani Mara kupitia miradi ya ujirani mwema inayotekelezwa na Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA).


NA ARODIA PETER

UJANGILI uliokuwa unafanywa na baadhi ya wenyeji wanaopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara umedhibitiwa kisayansi kupitia miradi ya kijamii na kiuchumi inayotekelezwa na hifadhi hiyo.

Miradi hiyo ya ujirani mwema (SCIPs) inatekelezwa na Shirika la Hifadhi ya Taifa (TANAPA) kwenye vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa Serengeti ambayo imetajwa kuwa chachu ya kupunguza vitendo vya ujangili, uingizaji mifugo kwenye hifadhi na kuwa tishio kwa wanyamapori na mazingira.


Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea hifadhi hiyo Juni 19, 2025, Ofisa Mahusiano ya Jamii wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Abed Mwesigwa alisema jumla ya miradi 181 imetekelezwa kwenye Wilaya za Serengeti, Bunda, Tarime, Busega, Bariadi, Itilima, Meatu na Ngorongoro katika mikoa ya Mara, Arusha na Simiyu yenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 300.


Miradi hiyo ni pamoja na miundombinu ya afya, elimu, maji, barabara na madaraja huku pia wakitekeleza mradi wa matumizi bora ya ardhi kwa kushirikiana na wadau wengine.


Mbali na hilo, Mwesigwa alisema baadhi ya vijana katika vijiji hivyo wamekuwa wakipatiwa ajira mbalimbali kwenye kampuni za ulinzi na uwindaji ili kuwainua kiuchumi na hivyo kushiriki ulinzi wa raslimali za taifa.


Kwenye miradi hiyo, TANAPA wamejenga shule, kuchimba mabwawa ya maji kwa ajili ya mifugo, nyumba za madaktari katika baadhi ya zahanati, nyumba za walimu, bweni la wanafunzi wa kike, barabara madaraja pamoja na ujenzi wa vito vya askari kwa ajili ya ulinzi wa Wanyama wakali katika vijiji jirani na hifadhi.


Hata hivyo, shirika hilo limeweka masharti kadhaa ya utoaji miradi hiyo ikiwa ni pamoja na vijiji husika kutokomeza ujangili pamoja na kuacha kuingiza mifugo kwenye hifadhi kwa ajili ya malisho ili kulinda ikolojia ya hifadhi.


Ofisa huyo alisema mbinu hiyo imekuwa chachu ya utulivu kwenye hifadhi kwani kila kijiji hivi sasa kinashindana kutokomeza vitendo hivyo haramu ili kukidhi vigezo vya kupata miradi ya maendeleo.


"Kijiji kinachoshiriki vitendo vya ujangili na uingizaji mifugo kwenye hifadhi, kinakosa sifa ya kupewa miradi hiyo, kutokana na kigezo hicho wanavijiji wamekuwa wanadhibitiana wenyewe na kupunguza ujangili hali inayowapatia manufaa zaidi.


“Ikumbuke kuwa hawa majangili wanaotoka mbali na maeneo hayo hawawezi kufanya vitendo hivyo bila kushirikiana na wenyeji.”alisema Mwesigwa.


Kwa mujibu wa Mwesigwa, Hifadhi ya Serengeti imezungukwa na vijiji 248 vilivyopo katika wilaya nane za mikoa mitatu ya Arusha, Mara na Simiyu na vyote vimeweza kufikiwa na kunufaika na miradi hiyo.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Bokore, Nelson James alikiri Kijiji chake kujengewa zahanati ya kisasa yenye thamani ya zaidi ya milioni 400 sambamba na barabara yenye urefu wa kilometa 12 ambayo ilikuwa haipitiki hasa wakati za masika.


"Zahanati hii ni mkombozi mkubwa kwa wajawazito, sasa tunao uhakika wa kupata huduma saa 24”alisema Nyabikwabe Nyerera mkazi wa Kijiji cha Bokore.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI