Header Ads Widget

RAIS SAMIA KUTEGUA KITENDAWILI CHA UPATIKANAJI WA MAJI SAFI NA SALAMA JIJINI MWANZA

 

Na Chausiku Said — Matukio Daima, Mwanza

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa serikali imejidhatiti kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Jiji la Mwanza na viunga vyake.

Akizungumza leo, Juni 20, 2025, wakati wa uzinduzi wa chanzo kipya cha maji cha Butimba, kilichogharimu Shilingi bilioni 71, Rais Samia alieleza kuwa uwepo wa maziwa makuu yakiwemo Ziwa Victoria ni rasilimali muhimu katika kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji kwa matumizi ya kijamii na kiuchumi.

“Hivyo ni vyema tukazingatia uhifadhi wa mazingira, ikiwemo kupambana na kuenea kwa magugu maji Ziwa Victoria. Hili litahakikisha ziwa linaendelea kuwa chanzo endelevu cha maji, na kuwezesha shughuli za maendeleo kama kilimo, ufugaji, uvuvi na utalii,” alisema Rais Samia.




Rais Samia alisisitiza kuwa huduma ya maji safi na salama ina gharama kubwa, hivyo wananchi wanapaswa kulipa bili za maji kwa wakati, huku akisisitiza watumishi wa mamlaka za maji kuwapatia wananchi ankara halali ili kuepusha malalamiko ya bili kubwa zisizoeleweka.

Chanzo hicho cha kisasa cha Butimba kinatarajiwa kuboresha huduma ya maji kwa zaidi ya wakazi 45,000 wa Jiji la Mwanza na maeneo jirani. Aidha, mradi huo umehusisha ujenzi wa matanki ya kuhifadhi maji katika maeneo ya miinuko na ujenzi wa mfumo wa uchakataji wa maji taka katika Gereza la Butimba.

Akitoa taarifa ya utekelezaji, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, alisema mahitaji ya maji kwa Mkoa wa Mwanza ni lita milioni 172 kwa siku, wakati uzalishaji wa sasa ukiwa ni lita milioni 138 kutoka vyanzo vya Capripoint na Butimba.


Huduma ya maji katika Mkoa wa Mwanza inasimamiwa na taasisi tatu: Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), SEWASA kwa Wilaya ya Sengerema, na RUWASA kwa maeneo ya vijijini.

Kwa upande wa takwimu za maendeleo ya huduma ya maji safi, Mkoa wa Mwanza umeongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kutoka asilimia 57 mwaka 2021 hadi asilimia 85 mwaka 2025. Wilaya mbalimbali pia zimeonyesha mafanikio makubwa: Misungwi (12% hadi 90%), Magu (55% hadi 93.3%), Sengerema (61% hadi 92%), Ilemela (80% hadi 90%), Nyamagana (59% hadi 78%), Ukerewe (69% hadi 81%), na Kwimba (67% hadi 78%).

Naye Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alibainisha kuwa kati ya vijiji 12,318 vilivyokuwa havina huduma ya maji nchini, serikali ya Rais Samia tayari imefikisha huduma hiyo katika vijiji 10,576 ndani ya kipindi cha miaka minne, na sasa vimebaki vijiji 1,500 tu ambavyo bado havijafikiwa.

Ameongeza kuwa moja ya kilio kikuu cha wakazi wa Mwanza kilikuwa ni matumizi ya Ziwa Victoria kutatua changamoto ya maji, hatua ambayo sasa imepata suluhisho kupitia mradi huu mkubwa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI