Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MBUNGE wa jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma Felix Kavejuru amesema kuwa ametekeleza wajibu wake kikamilifu katika kuchochea miradi ya maendeleo iliyofanikisha kutekelezwa kwa miradi ya maendeleo ambayo inagusa maisha ya wananchi wa jimbo hilo moja kwa moja.
Kavejuru alisema hayo akihutubia mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Kibande wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma kilichopo mpakani na nchi ya Burundi ikiwa ni mkutano wake wa mwisho kabla kuanza kwa mchakato wa uchaguzi Mkuu ambapo ametangaza pia azma yake ya kugombea tena katika jimbo hilo.
Mbunge huyo ambaye alishinda nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Dk.Philip Mpango aliyeteuliwa kuwa Makamu wa Raisi alisema kuwa katika kipindi cha miaka mine aliyokuwa mbunge katika jimbo la Buhigwe amewezesha kujengwa kwa zahanati 15 sambamba na vituo vya afya vipya vinne ambapo mfuko wa jimbo umekuwa na mchango mkubwa katika kukamilisha miradi hiyo.
Alisema kuwa pamoja na miradi hiyo amewezesha utekelezaji wa miradi ya maji ambapo wakati anaingia kati ya vijiji 39 vya jimbo hilo ni vijiji vitatu ndiyo vilivyokuwa na miradi ya maji ambapo kwa sasa vijiji vyote vina miradi ya maji na sehemu kubwa ya miradi hiyo imeashaanza kutoa huduma ikiwemo mradi wa vijiji vinane wenye thamani ya shilingi Bilioni 9.7 utakaotoa huduma kwa wananchi 79,4000 wa jimbo hilo.
Akizungumza katika kijiji hicho Mwenyekiti wa kijiji cha Kibande wilaya ya Buhigwe, Morodekai Mazibwe alisema kuwa wananchi wa kijiji hicho wameshiriki kwenye miradi mbalimbali iliyotekelezwa wakati wa kipindi cha Mbunge huyo ukiwemo mradi wa maji wenye thamani ya Zaidi ya shilingi Bilioni moja ambapo wananchi walichangia mawe, matofali na mchanga.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo alisema kuwa bado barabara zinazoingia na kutoka kwenye kijiji hicho zipo kwenye hali mbaya hivyo kuiomba serikali kuliangalia jambo hilo kwani linakwamisha mchango wa maendeleo katika kuwafanya wanakijiji kusafirisha mazao yao.
0 Comments