Kutiwa saini kwa makubaliano ya amani kati ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda mjini Washington kumezua hisia tofauti, huku rais wa zamani wa Congo, Joseph Kabila, akieleza kuwa "si chochote zaidi ya makubaliano ya kibiashara".
Mkataba huo uliotiwa saini siku ya Ijumaa ulidai "kutengwa, kupokonywa silaha na kuunganishwa kwa masharti" kwa vikundi vyenye silaha vinavyopigana mashariki mwa DR Congo - lakini ulitoa maelezo mengine machache.
Huku wengine kama vile Kabila wakipinga makubaliano hayo, wengine wamepongeza makubaliano hayo kama hatua ya mabadiliko katika mzozo mbaya ambao umeendelea kwa miongo kadhaa.
Rwanda imekanusha madai kuwa inaunga mkono kundi lenye silaha, linalojulikana kwa jina la M23, ambalo limekuwa likipigana mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mzozo huo uliongezeka mapema mwaka huu wakati waasi wa M23 walipochukua udhibiti wa maeneo makubwa ya mashariki mwa DR Congo, ikiwa ni pamoja na mji mkuu wa eneo hilo, Goma, mji wa Bukavu na viwanja vya ndege viwili.
Umoja wa Mataifa unasema maelfu ya watu wameuawa na mamia kwa maelfu ya raia kulazimishwa kutoka makwao kufuatia mashambulizi ya hivi majuzi ya waasi.
M23 inapinga takwimu hizo, ikisema ni chini ya watu 1,000 wamefariki.
Baada ya eneo hilo kutekwa, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo iliigeukia Marekani kwa msaada, ikiripoti kutoa upatikanaji wa madini muhimu badala ya dhamana ya usalama.
Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuna utajiri wa coltan na rasilimali nyingine muhimu kwa tasnia ya kimataifa ya vifaa vya elektroniki.
0 Comments