Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajia kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya kitaifa ya siku ya watu wenye ualbino yanayotarajia kufanyika Juni 13 mwaka huu mkoani Kigoma akimwakilisha Raisi Samia Suluhu Hassan.
Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kigoma ambapo amewataka wananchi wa mkoa Kigoma kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho yanayofanyika Uwanja wa Mwanga Community Centre mjini Kigoma.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa mkoa Kigoma akizungumza wakati wa kufanya usafi kwenye kituo cha kulea wazee mjini Kigoma ikiwa sehemu ya maadhimisho hayo ametoa wito kwa wananchi hao kuachana na Imani na mila potofu zinazowanyanyapa na kuwafanyia ukatili watu wenye ualbino mambo ambayo yanahatarisha maisha yao.
Ametaka jamii iwashirikishe watu wenye ualbino kwenye mipango mbalimbali ya maendeleo kwani kama binadamu wengine wanao mchango mkubwa kwenye maendeleo.
Kwa upande wake Raisi wa Chama cha Watu wenye ualbino, Godson Mollel amekemea tabia ya baadhi ya watu kuwaona watu wenye ualbino kama watu wa ajabu ambao hawastahili kuishi na ndiyo maana wanawafanyia matendo yasiyofaa ikiwemo kuwakata viungo kwa ajili ya masuala ya ushirikina.
Mollel alisema kuwa siku ya Watu Wenye ualbino imenzishwa maalum kwa ajili ya kutoa elimu na uelewa kuhusu jamii hiyo kwamba ni watu kama watu wengine wakiwa na mchango kwenye jamii kama walivyo binadamu wengine
0 Comments