Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA
ALIYEKUWA Makamu Mwenyekiti Chadema Kanda ya Kati, Jackison Jingu, amevitaka vyama vya siasa kufanya siasa za kistaarabu kwa kueleza sera kwa wananchi badala kufitinishana hali inayoweza kusababisha kuvunjika kwa amani na utulivu nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo (7/6/2025) alisema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa kuchagua Rais,wabunge na madiwani kunahitajika kuendesha siasa nzuri kwa kuelezea sera ambazo zitaweza kushawishi wananchi kukichagua chama husika.
"Siasa wanazofanya hivi sasa Chadema na Chauma wanafitinishana hawaelezi sera za vyama vyao haya mambo hayana afya kwa taifa na yakiachwa kimsingi yanaweza kusababisha kuvunjika kwa amani," alisema Jingu ambaye alisema bado anatafakari chama cha kujiunga nacho baada ya kuachana na Chadema.
Jingu alisema kuwa chama makini hakihitaji kuona siasa za kuchukiana, matusi au kutupiana maneno machafu bali siasa za kistaarabu zitakazowajenga viongozi na kuwashawishi wananchi kwa hoja, si kwa mabavu au mivutano isiyo na tija.
Amesema hakuna sababu ya kuchukiana kwa sababu ya siasa, kwani ushindani ni wa muda na demokrasia inaruhusu tofauti za mawazo.
Alisema mivutano inayoendelea kati ya Chadema na Chauma katika mikutano inayofanywa na viongozi wa chama hicho ndio inaipa uimara CCM ambayo imekuwa ikizingatia misingi ya kidemokrasia na kufuata taratibu zake, ikiwemo kurudi kwa wananchi kila baada ya miaka mitano ili kuomba ridhaa upya.
Jingu ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Singida, alisema viongozi wa vyama vya upinzani wanastahili kumheshimu rais Dk.Samia Suluhu Hassan hata kama ni mwanamke kwani ndio rais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania.
0 Comments