NA MATUKIO DAIMA MEDIA
Kada wa chama cha mapinduzi na mwanachama wa umoja wa vijana wa chama hicho (UVCCM) mkoa wa Iringa Jasmin Ng’umbi leo amejitokeza katika ofisi za UVCCM mkoani humo kuchukua fomu ya kugombea ubunge vijana Taifa.
Akizungumza na Matukio Daima mara baada ya kuchukua fomu hiyo Jasmin Ng’umbi amesema kuwa amechukua uamuzi huo baada ya kujipima na kujiridhisha kuwa anatosha kuwawakilisha vijana bungeni hivyo kama atapata ridhaa baada ya kuchukua fomu hiyo atahakikisha anasimama vizuri katika nafasi atakayoaminiwa.
Jasmin amesema kuwa serikali chini ya chama cha mapinduzi CCM imekuwa ikiwaamini vijana katika nafasi mbalimbali za uongozi hivyo ni wakati wa vijana kuchangamkia fursa za kugombea nafasi mbalimbali kwa kuwa kila mmoja anahaki ya kuchagua na kuchaguliwa katika uongozi.
‘’Niwahamasishe vijana wenzangu kujitokeza kuchukua fomu za kugombea vijana tunaweza na tunaaminiwa sana na serikali, mfano mzuri tunao kama vijana wengi nchini walioaminiwa na Rais Dkt Samia"
Aidha Jasmini aliwataka vijana wote watakaoaminiwa kushika nafasi za uongozi kufanya kazi kwa uaminifu na kuzingatia kanuni na Katiba ya nchi katika kusimamia ilani ya chama cha mapinduzi ambayo imetambulishwa hivi karibuni itakayotumika kwa miaka mitano 2025/2030.
Jasmin pia aliwahamasisha wananchi kujitokeza katika kushiriki kampeni za amani pindi zitakaporuhusiwa Pamoja na kujitokeza katika zoezi la kupiga kura katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika oktoba 2025.
Zoezi la kuchukua na kurudisa fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi za ubunge na udiwani ndani ya CCM limeanza leo June 28 na litafikia ukomo Julai 2 mwaka huu huku waliojitokeza kuchukua fomu hizo wakiaswa kufuata muongozo wa kanuni za uteuzi zilizowekwa.
katibu wa UVCCM mkoa wa Iringa Aisha Mpuya aliwata vijana wenye sifa na nia ya ubunge kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu hizo.
Alisema gharama ya fomu ya ubunge ni Tsh 500,000 na kuwa zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu litafungwa Julai 2 saa 10:00 jioni.
Aisha alisema kuwa vijana wasiwe nyuma wajitokeze katika nafasi za ubunge wa majimbo,ubunge wa viti maalum pamoja na udiwani wa kata na udiwani wa viti maalum.
0 Comments