Header Ads Widget

IDADI YA WALIOACHWA BILA YA MAKAZI HAITI YAVUNJA REKODI

Takwimu mpya za Umoja wa Mataifa zinasema idadi ya watu walioachwa bila ya makazi Haiti imevunja rekodi.

Tangu mwezi Desemba idadi hiyo imeongezeka kwa asilimia 24 ikifikisha idadi jumla ya walioachwa bila ya makazi Haiti kupindukia milioni 1.3.

Mji mkuu wa Port-au-Prince ndiyo ulioathirika zaidi lakini pia ghasia zimezagaa hadi kwa miji mingine ya nchi hiyo.

Magenge ya wahalifu yanadhibiti maeneo mengi ya mji huo ikiripoti kuwa magenge hayo yameungana na sasa yanadhibiti asilimia 85 ya mji mkuu.

Umoja wa Mataifa unasema watu hao milioni moja nukta tatu walioachwa bila ya makazi ndiyo idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa Haiti, taifa linalokumbwa na ghasia kali kwa miaka mingi.

Mauaji, ubakaji, utekaji nyara na uporaji vimechangia pakubwa katika kulitumbukiza taifa hilo katika msukosuko wa kisiasa.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la uhamiaji la IOM Amy Pope ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kudhibiti hali akisema watu wamelazimika kuyahama makazi yao mara kadhaa na mzozo huo haupaswi kuchukuliwa kuwa hali ya kawaida.

Pope ameongeza kuwa waathiriwa wanapitia dhiki na mateso yasiolezeka na wengi wao hawana chochote na wanaishi katika mazingira yasiyo salama na kwenye mahema bila ya mahitaji muhimu kama huduma za afya, maji safi ya kunywa, chakula cha kutosha na elimu kwa watoto wao.

Robo ya walioachwa bila ya makazi wanaishi mjini Port au Prince lakini idadi ya wanaokimbilia katika maeneo mengi ya nchi inazidi kuongezeka.

IOM inasema idadi ya walioachwa bila ya makazi kaskazini mwa Haiti imeongezeka kwa asilimia themanini.

Mnamo mwezi Februari, shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto UNICEF, liliripoti ongezeko la visa vya unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto.

Umasikini mkubwa pia umewafanya watoto wengi kujiunga na magenge ya wahalifu.

UNICEF inasema nusu ya idadi ya wapiganaji wa magenge hayo ni watoto.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI