Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano na serikali ya Ubelgiji zimeanza utekelezaji wa pamoja wa kuimarisha madawati ya jinsia kwenye vyuo vya ufundi mkoani Kigoma lengo likiwa kuhakikisha vijana wenye umri wa miaka 14 hadi 29 wanastawi katika mazingira ya ulinzi jumuishi na usawa wa kijinsia.
Hayo yanakuja baada ya kuzinduliwa kwa madawati ya jinsia kwenye vyuo vya ufundi stadi mkoani Kigoma sambamba na uzinduzi wa utoaji mafunzo ya elimu ya jinsia katika mradi wa miaka mitano wenye thamani ya shilingi Bilioni 77 utakaotekelezwa kwenye wilaya tano za mkoa Kigoma.
Mradi huo unatekelezwa kwa ushirkiano baina ya Shirika la Maendeleo la Ubelgiji (ENABEL) na serikali ya tanzania kupitia halmashauri za mkoa Kigoma kupitia mradi wa wezesha Binti ambapo vijana zaidi ya 2300 wanatarajia kufaidika na mpango huo.
Akizungumza katika uzinduzi huo Meneja wa Mradi wa Wezesha Binti kutoka Shirika la Enabel, Robert Kisalama alisema kuwa Mantiki ya kuzindua dawati la jinsia katika vituo vya mafunzo ya ufundi stadi ni kukuza usawa wa kijinsia, kushughulikia unyanyasaji wa kijinsia (GBV), na kuunda mazingira salama na jumuishi ya kujifunza ili kuwezesha kuongezeka kwa upatikanaji wa ajira zinazostahili na ujasiriamali kwa wasichana na vijana.
Akizindua dawati hilo katika uzinduzi uliofanyika chuo cha VETA Kigoma, Katibu Tawala wa mkoa Kigoma,Hassan Rugwa alisema kuwa anaamini uzinduzi wa madawati ya jinsia kwenye vyuo vya ufindi na vyo vya elimu ya kati na juu mkoani Kigoma kutachochea utekelezaji wa mpango wa serikali katika kusimamia usawa wa kijinsia kwenye maeneo yote.
Rugwa alisema kuwa anaamini kuwa wanafunzi watakaopitia kwenye mpango huo watakuwa mabalozi wazuri kwenye jamii zao katika kupunguza suala zima la ukatili kwenye jamii ambalo haliwapati wanawake pekee yao lakini pia linahusika na jamii nzima japokuwa wanawake na watoto ndiyo waathirika wakubwa wa vitendo hivyo.
0 Comments