Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mkoani Songwe Mheshimiwa Farida Mgomi, amewataka wananchi wilayani humo kuwa na utamaduni wa kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na kufanya usafi wa maeneo yanayowazunguka na kulinda vyanzo vya maji ili kuhakikisha usafi na usalama wa mazingira unaimarika.
Akizungumza wakati wa kilele cha wiki ya Mazingira katika Kijiji cha Msia, Kata ya Chitete Ileje, Mhe. DC Mgomi amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki katika juhudi za kudhibiti uharibifu wa mazingira, sambamba na kuacha matumizi holela ya plastiki, kama inavyoelekezwa katika kaulimbiu ya mwaka huu isemayo “Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo, Tuwajibike Sasa – Dhibiti Matumizi ya Plastiki”.
Aidha, DC Mgomi almwaagiza maafisa Mazingira katika wilaya hiyo kuhakikisha wanakuwa na mipango kazi madhubuti pamoja na mikakati ya kudumu ya kusimamia, kuratibu na kuzuia uharibifu wa mazingira katika maeneo yao ya kazi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha usafi hausubiri maadhimisho pekee baliniwe tabia ya kila mara.
Maadhimisho hayo yalipambwa na vikundi vya burudani mbalimbali zikiwemo ngoma za asili huku wananchi wakionesha ushirikiano mkubwa katika shughuli za usafi na uelimishaji wa mazingira kwa ujumla wake.
0 Comments