Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limekamilisha rasmi shughuli zake tarehe 27 Juni 2025 kwa Rais Samia Suluhu Hassan kulihutubia. Bunge hilo litavunjwa rasmi Agosti 03, 2025 litakapokamilisha kipindi chake kikatiba. Baada ya hatua hiyo itafungua rasmi dirisha la kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025. Katika uchaguzi huo, Watanzania watawachagua madiwani, wabunge, na Rais.
Hata hivyo, chama kikuu cha upinzani nchini, CHADEMA, kikiongozwa na Mwenyekiti wake Tundu Lissu, kimeendelea kushikilia msimamo wa kupigania mageuzi ya sheria za uchaguzi kabla ya uchaguzi kufanyika. Kupitia vuguvugu yao maarufu ya No Reforms No Election, CHADEMA kinadai kuwepo kwa mazingira huru, haki, na sawa ya uchaguzi.
Katika kauli yake, Lissu alisema: "Tunataka mabadiliko ya mfumo wetu wa uchaguzi. Hatutaki mfumo utakaoipendelea CHADEMA au unaoipendelea CCM, tunataka mfumo ulio huru."
"Kupiga kura hakuna maana tena, kura haina thamani yoyote kuamua mwenyekiti, diwani, mbunge au rais. Tumechoka kudhulumiwa kweli, tupiganie mabadiliko, tusisimamiwe uchaguzi na mfumo huu," alisema Lissu akiwa Iringa siku chache kabla ya kukamatwa kwa tuhuma za uhaini.
Mabadiliko yanayotakiwa na CHADEMA
Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu, akiwa Mahakamani kwa kesi ya uhaini amevalia fulana iliyoandikwa "No Reforms No Election" kudai mabadiliko
Pamoja na vyama vingine kama ACT-Wazalendo, CHADEMA imekuwa ikisisitiza haja ya mabadiliko makubwa ya mfumo wa uchaguzi, ambayo ni pamoja na:
-Kuundwa kwa Tume huru ya uchaguzi inayojitegemea kweli
-Uchaguzi usisimamiwe na wakurugenzi wa halmashauri
-Wagombea kupita bila kupingwa
-Ushiriki wa wagombea usizuiwe kwa sababu zisizo za msingi
-Kuwepo kwa mazingira ya usawa kwa mawakala wa vyama
-Matokeo ya urais yaweze kuhojiwa mahakamani
-Kuzuia kura feki na vituo hewa
-Vyombo vya ulinzi visiingilie uchaguzi
Kati ya masuala mengi, suala linalotajwa sana ni kuhusu uhuru wa Tume huru ya taifa ya uchaguzi. "Mtakubaliana na mimi, kwamba uchaguzi mambo yanayolalamikiwa, hata No reform No election, mambo makubwa karibu aslimia 90 yanagusa tume huru ya taifa ya uchaguzi…anasema Deus Kibamba, mchambuzi wa siasa Tanzania.
Lissu na CHADEMA wameendelea kushikilia kuwa mfumo uliopo sasa unakipendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na kuwa tume, sheria, na taratibu zote zimo chini ya ushawishi wa chama hicho.
Chama hicho kikuu cha upinzani kinasema kutokana na mfumo wa sasa wanaouita 'mbovu', katika miaka 10 iliyopita chama hicho kilishinda vijiji 1,754 lakini sasa kina vijijini 97, na kutoka wabunge 75 sasa wana mbunge mmoja.
Mabadiliko yaliyofanyika
Ado November, Mwenyekiti wa Bodi ya chama cha Mawakili wa serikali
Licha ya msimamo wa CHADEMA, Serikali kupitia Bunge la 12 ilipitisha miswada mitatu mikuu inayohusiana na uchaguzi: Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2023, Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 2023, na Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa ya mwaka 2023.
Katika kongamano la kitaifa la sheria lililofanyika hivi karibuni, Ado November, Mwenyekiti wa Bodi ya chama cha Mawakili wa serikali, alisema:
"Serikali imefanya maboresho katika sheria za uchaguzi, hivyo asitokee mtu akaongelea kuwa serikali haijafanya uboreshaji wowote."
Alitaja mabadiliko hayo kuwa ni pamoja na:
-Kuwepo kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) yenye sheria yake maalum
-Uwezekano wa kesi za uchaguzi kumalizika ndani ya miezi sita
-Kuondolewa kwa wakurugenzi wa halmashauri kama wasimamizi wa uchaguzi
-Watumishi wa umma wenye sifa kusimamia uchaguzi kwa niaba ya INEC
-Uwazi katika uteuzi wa wajumbe wa tume kupitia usaili na mapendekezo kwa Rais
-Wafungwa kuruhusiwa kupiga kura kwa mara ya kwanza
Akilihutubia Bunge, Rais Samia amesema: "Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, Tume Huru ya Uchaguzi iliundwa kwa sheria yake yenyewe. Tulifanya hivi ili kujibu rai ya muda mrefu ya wadau wa kisiasa".
Amesema pia Sheria mpya ya Uchaguzi imeongeza takwa la mgomnea kupigiwa kira ya hapana kama amebaki peke yake, wengine wameondolewa ama amejitokea mgombea mmoja pekee kuwania nafasi husika.
"Hatua hii inafuta kilichojulikana kama anapita bila kupingwa," anaswma Rais Samia.
Wakili Francis Stolla aliongeza kuwa sheria mpya inaruhusu uteuzi wa wajumbe wa tume kufanywa kwa njia ya uwazi na usaili, na kwamba hatua hizo zinaonyesha uboreshaji mkubwa.
Mjadala na mashaka
Mchambuzi wa siasa, Deus Kibamba
Pamoja na mabadiliko hayo, baadhi ya wadau wanaendelea kuwa na mashaka na dhamira ya serikali. Wanasema mabadiliko yamefanyika lakini kuna mahali yalipaswa kuboreshwa zaidi, ikiwemo ya watumishi wa umma kuendelea kuwa sehemu ya uchaguzi na mamlaka ya Rais kwenye uteuzi wa watumishi wa tume.
Mchambuzi wa siasa Deus Kibamba alizungumzia uwepo wa mmoja wa makamishna wa Tume huru ya uchaguzi (INEC) mpya iliyoundwa kwa sheria mpya, ana historia ya kuwa kiongozi wa chama cha siasa, jambo linalotia mashaka juu ya uhuru wa tume hiyo.
Kibamba anasema pamoja na mabadiliko yaliyofanywa, anasema yako masuala kadhaa ambayo yanaweza kubadilishwa bila kugusa mabadiliko ya sheria na katiba.
"Nimesoma sheria, katiba yetu, sheria ya uchaguzi, sheria ya tume huru, nikabaini mambo yanayotakiwa yashughulikiwe kati ya sasa na uchaguzi ni 97. Zaidi ya nusu ya hayo, mambo 50, hayahitaji mabadiliko ya sheria wala katiba."
Pamoja na mashaka waliyonayo baadhi ya wadau, hotuba ya ya Rais ya kuhitimisha shughuli za bunge imeonyesha dhamira ya kufanya mabadiliko kwa upana wake kwa kuendeleza ama kuanzisha mchakato wa katiba mpya uliokwama kwa zaidi ya miaka 10. Inawezekana isikidhi kilio cha CHADEMA kuelekea uchaguzi wa Oktoba, ila ukaanzisha mjadala mpana kuelekea uchaguzi wa 2030, na chaguzi zingine zijazo.
"Mapendekezo yao mengi yamepokewa na kufanyiwa kazi. Kwa kuwa takwa la kikatiba ni jambo la muda mrefu la Tume ya Maridhiano, mchakato wa katiba mpya ni sehemu ya Ilani ya CCM 2025–2030, hivyo shughuli ya kuanza mchakato huo itafanyika katika kipindi kijacho cha miaka mitano," anasema Rais Samia.
Je, kuna mwanya wa mabadiliko sasa baada ya Bunge kumaliza shughuli zake?
Spika wa Bunge la 12, Tulia Ackson akiwa na mgeni wake Rais Samia kuhitimisha shughuli za bunge hilo, Juni 27, 2025
Kwa mchambuizi Kibamba, anasema angalau nusu ya masuala 97 aliyoyabaini yanaweza kufanyiwa marekebisho bila kuhitaji bunge kukaa kujadili na kupitisha muswada wowote wa sheria.
Kwa mtazamo wa mwanasheria Edwin Mugambira yeye anasema bunge likivunjwa maana yake masuala yote makubwa ya kisheria kwa sasa mlango umefungwa.
"Kimsingi, baada ya kufungwa bunge tarehe 27, kutakuwa hakuna mwanya wowote wa kufanya mabadiliko makubwa ya kisheria, mchakato wa kisheria unafanyika kupitia bungeni, muswada ukishakubalika uende kwa rais aupitishe kama sheria, inawezekana kupitishwa kwa muda mfupi kwa hati ya dharura", anasema mwanasheria Edwin Mugambira.
Anaungwa mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) , Anna Henga anayeiambia BBC kwamba bunge likishavunjwa linakosa uhalali wa kuitishwa tena kwa mujibu wa katiba.
"Kwa hivyo mlango wa reforms umefungwa labda mpaka baada ya uchaguzi na bunge jipya, rais anaweza kuitisha bunge kama kuna dharura ya vita au nyingineyo lakini sio baada ya bunge kuvunjwa".
Hakuna anayejua kati ya sasa mpaka Agosti 03, 2025 kama bunge linaweza kuitishwa kwa dharura kabla ya kuvunjwa rasmi litakapokamilisha kipindi chake kikatiba.
Nafasi ya mazungumzo
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Stephen Wasira anasema kauli ya 'No Reform, No Election' ya Chadema haina nafasi kwa sasa
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Stephen Wasira, katika kauli yake ya Januari 2025 alisema:
"Kauli ya 'No Reform, No Election' haina nafasi kwa sasa. Rais Samia Suluhu Hassan na CCM wameonyesha utayari wa mazungumzo, na bunge linakaribia kuvunjwa, hivyo hakuna muda wa kufanya mabadiliko ya kisheria yanayohitaji muda mrefu."
Kauli hii aliyoitoa Wassira mwezi Januari, 2025, ni kauli ya CCM inayooongoza Serikali, ni kauli yenye nguvu, kwa nafasi yake kama mtu wa pili na kwa wadhifa kwenye chama baada ya Mwenyekiti ambaye ni Rais Samia. Kama mwezi Januari, chama tawala kiliona 'No Reform, No Election' haina nafasi, kwa muda uliosalia kati ya sasa mpaka Agosti 03, bunge litakapovunjwa rasmi, na kati ya sasa mpaka uchaguzi wa Oktoba, mabadiliko yatawezekana?
Ni swali muhimu lakini Mchambuzi Kibamba anasema "Mambo mengi yanahitaji mazungumzo," akisema inawezekana kufanyika mazungumzo kama kuna utashi wa kisiasa kwenye kufanya mabadiliko. Hilo analisema pia Mwanasheria Mugambira kwamba njia bora sasa ni hatua za kiutawala na mazungumzo.
Chadema ilishawahi kuwa na mikutano kadhaa ya maridhiano na chama tawala, CCM kinachoongoza serikali, hasa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani mwaka 2021. Lakini mazungumzo yaliishia njiani yakionyesha kulikuwa na tofauti ya kimtazamo baina ya pande mbili.
Lakini hali inazidi kuwa tata. Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ambaye sasa yuko rumande kwa tuhuma za uhaini, alishasema kupitia BBC: "Hakuna tena mazungumzo wala maridhiano."
Hivyo basi, kwa muda mfupi uliosalia kabla ya uchaguzi mkuu na mazingira yalivyo, hatma ya vuguvugu la No Reforms inaonekana kutokuwepo tena mikononi mwa sheria, bali ni utashi na maamuzi ya kisiasa yatakayoamua iwapo kutakuwa na mabadiliko, ushiriki mpana au kuendelea kususia uchaguzi.
Inaendelea kusubiriwa kama CHADEMA ambao mwenyekiti wao, Lissu anashikiliwa kwa kesi ya uhaini itageuza msimamo? Au historia ya uchaguzi wa 2025 itaandikwa bila wao kushiriki na kuzika matamanio yao ya mabadiliko angalau kwa sasa?
0 Comments