Na Matukio Daima Media
Ndege ya Air India namba AI 171 imeanguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ahmedabad, ikiwa na abiria 242, wakiwemo viongozi wa kisiasa.
Ndege hiyo, iliyokuwa ikielekea London, ilikuwa na jumla ya watu 242, wakiwemo marubani wawili na wahudumu 10 wa ndani ya ndege.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kutoka chombo cha habari nchini humo The Hindu Juni 12,2025 imeeleza kuwa ndege hiyo ilitoa wito wa dharura MAYDAY lakini ikapoteza mawasiliano mara moja baada ya hapo. Baada ya kupaa kutoka Runway 23 saa 7 mchana, ndege hiyo ilianguka nje ya uzio wa uwanja huo na kushika moto.
Moshi mzito mweusi ulionekana ukifuka kutoka eneo la ajali, huku shughuli za uokoaji zikiendelea kwa kasi. Serikali ya Gujarat imethibitisha kuwa Waziri Mkuu wa zamani wa jimbo hilo, Vijay Rupani, alikuwa miongoni mwa abiria waliokuwa kwenye ndege hiyo. Hali yake haijafahamika kwa sasa.
Katika juhudi za kuokoa maisha, serikali ya jimbo hilo imeanzisha "green corridor" maalum kati ya eneo la ajali na Hospitali Kuu ya Serikali, ili majeruhi wafikishwe haraka kwa matibabu. Pia, vikosi vya uokoaji vya kitaifa (NDRF) na vya jimbo (SDRF) vimepelekwa eneo la tukio kusaidia kazi ya uokoaji, uchunguzi na udhibiti wa madhara.
Mashirika ya usalama wa anga na usafiri wa India tayari yameanza uchunguzi rasmi kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Kwa sasa, bado haijafahamika ni watu wangapi wamepoteza maisha au kujeruhiwa, lakini mashuhuda wameeleza kuona mabaki ya ndege yaliyotapakaa na juhudi kubwa za kuokoa manusura.
0 Comments