Header Ads Widget

AFISA ELIMU JAMII (DCEA) ATOA ELIMU YA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA KWA MADEREVA WA BODABODA NA BAJAJI SAME


Na Ashrack Miraji Matukio Daima 

Afisa Elimu Jamii kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kanda ya kaskazini Shabani Miraji, amefanya ziara maalum katika vijiwe vitatu vya bodaboda wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, kwa lengo la kutoa elimu kuhusu madhara ya usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya.

Ziara hiyo ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kupambana na biashara haramu ya dawa hizo, hasa ikizingatiwa kuwa madereva wa bodaboda mara nyingi hutumiwa kama njia rahisi ya usafirishaji wa dawa hizo katika maeneo ya mijini na vijijini.

Katika hotuba yake kwa madereva wa bodaboda, Miraji alieleza kuwa kundi hilo ni muhimu sana katika jamii, lakini limekuwa likihusishwa na matukio ya kihalifu, hasa usafirishaji wa dawa za kulevya. Alisisitiza kuwa madereva wa bodaboda wana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko chanya endapo watakataa kushiriki katika biashara hiyo haramu.


"Tumejiridhisha kuwa baadhi ya watu wenye nia ovu hutumia madereva wa bodaboda kama njia ya kupitisha dawa za kulevya kwa sababu ya urahisi wa usafiri wao. Tunawaomba muache mara moja kushiriki vitendo hivyo kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa jamii nzima," alisema Miraji mbele ya mamia ya waendesha bodaboda waliohudhuria mkutano huo.

Afisa huyo alitumia nafasi hiyo kueleza madhara mbalimbali ya dawa za kulevya, yakiwemo kupoteza nguvu kazi ya taifa, kuongezeka kwa uhalifu, na kuvunjika kwa familia nyingi. Alisema kuwa elimu kwa jamii ni silaha muhimu katika mapambano dhidi ya matumizi na usafirishaji wa dawa hizo.

Wakati wa ziara hiyo, baadhi ya waendesha bodaboda walikiri kuwa wamekuwa wakishawishiwa mara kwa mara kusafirisha mizigo wasiyoijua, huku wakipewa ahadi ya malipo makubwa. Hata hivyo, wengi wao walikubali kuwa hawakuwa wakifahamu hatari zinazohusiana na vitendo hivyo.


Pia yalifanyika majadiliano ya wazi kati ya maafisa kutoka DCEA na madereva wa bodaboda na bajaji ambapo walisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa kwa mamlaka pindi wanapohisi kuna shughuli za dawa za kulevya katika maeneo yao.

Kwa kumalizia, Shabani Miraji aliwahimiza waendesha bodaboda na bajaji kuwa mabalozi wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kushirikiana na vyombo vya dola pamoja na kuelimishana wao kwa wao. Alisisitiza kuwa jukumu la kupambana na janga hilo ni la kila mmoja, na sio serikali pekee.



 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI