Header Ads Widget

WAZIRI NDUMBARO, MSONGAMANO KWENYE MAGEREZA KUENDELEA KUPUNGUA

  Na Lilian Kasenene, Morogoro Matukio DaimaApp 

WAZIRI wa Katiba na Sheria Dk Damas Ndumbaro amesema Wizara yake imeendelea kutembelea na kukagua Magereza mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha suala la msongamano kwenye Magereza hayo linapungua

Dk Ndumbaro alizungumza hayo mkoani Morogoro katika ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa sheria wa jeshi la magereza kuhusu huduma za msaada wa kisheria,mapokezi ya wafungwa magerezani na adhabu mbadala.

Waziri Ndumbaro alisema kuwa idadi hiyo imepungua baada ya kuimarisha adhabu mbadala kwa mahabusu.

"Wizara kupitia ofisi ya Taifa ya mashtaka inaendelea kukagua Magereza kwa lengo la kuainisha changamoto za kiutendaji na kiupelelezi, na katika Mwaka 2024/2025 Hadi kufikia Machi 2025  Magereza 132 yamekaguliwa ikilinganishwa na Magereza 107 yaliyokaguliwa 2023/2024 sawa na ongezekonla Magereza 23,"alisema Waziri huyo.

Alisema katika ukaguzi huo jumla ya mahabusu 618 waliachiwa lengo likiwa ni kupunguza msongamani.

Akizungumzia suala la Teknolojia ya habari na mawasiliano(Tehama) Dk Ndumbaro alisema kuwa Serikali kupitia wizara ya Katiba na Sheria imeendele kutoa vifaa vya TEHAMA vya kuendesha mahakama mtandao gerezani kwaajili ya kurahisisha usikilizaji wa mashauri ya wafungwa na watu wenye changamoto ya usafiri wa kwenda mahakamani.

Aidha,aliwataka maafisa Sheria wa   wa Magereza kuwa na wajibu wa kutoa msaada wa kisheria kwa wafungwa na mahabusu,ikiwa ni pamoja na kushughulikia mapokezi ya wafungwa kwa mujibu wa Sheria,pamoja na kushiriki katika kuandaa taarifa za wafungwa na hata mashauri ya kinidhamu,ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Aidha, alihimiza maafisa sheria hao kutumia siku hizo tano vya mafunzo kwa umakini mkubwa, wakitambua kuwa elimu watakayopata ni sehemu ya utekelezaji wa Mama Samia Legal Campaign inayolenga kuboresha upatikanaji wa haki nchini.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, kuanzia Julai 2024 hadi Aprili 2025, watu 68 waliokuwa wamehukumiwa kifungo wakiwa na matatizo ya afya ya akili wameachiwa huru, hatua iliyoleta nafuu kubwa katika kupunguza idadi ya wafungwa.

Naibu katibu mkuu wa wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Dk Maduhu Kazi alisema kuwa Wizara hiyo kwa kushirikiana na Magereza imeendelea kuboresha urekebu Magerezani 

Dk Maduhu Kazi, alieleza kuwa serikali pia imejipanga kuhakikisha mlundikano wa wafungwa na mahabusu unapungua kwa kiasi kikubwa.

"Kwa kipindi cha Januari hadi Aprili 2025, kumekuwa na wafungwa na mahabusu 27,000 ikilinganishwa na  32,000 mwaka 2021," alisema

Naye Kamishna Jenerali wa Magereza, Jeremia Matundu, alisema kuwa ndani ya Jeshi la Magereza kuna wanasheria zaidi ya 264, lakini ni 120 pekee waliopata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo na kwamba ni muhimu kwa kuwaongezea ujuzi, kubadilishana uzoefu na kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

“Tunatarajia waliopata mafunzo haya watafanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuwa walimu kwa wenzao ambao hawakushiriki,” alisema Matundu, na kuongeza kuwa jeshi la magereza litaendelea kutoa mafunzo ya aina hiyo kwa maafisa na wataalamu wake ili kwenda sambamba na maendeleo ya kiteknolojia.

Alisema kwa sasa, jumla ya magereza 66 nchini yana huduma ya mahakama mtandao, lakini bado kuna wilaya 50 zisizo na magereza, hivyo kusababisha baadhi ya watuhumiwa kupelekwa katika wilaya jirani lakini mkakati wa Serikali ni kuongeza idadi ya magereza ili kuhakikisha kila wilaya inakuwa na kituo chake.

Mkurugenzi wa Idara Katiba na Ufuatiliaji wa Haki Jane Lyimo alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kupunguza wafungwa na mahabusu magerezani, kuimarisha umahiri wa maafisa na kuboresha utendaji wa haki kwa wafungwa hao.


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI