Na Lilian Kasenene,Morogoro
Jeshi la polisi mkoa wa Morogoro linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za mauaji katika matukio tofauti yaliotokea huko Ruhembe wilayani Kilosa.
Kamanda wa polisi mkoani Morogoro Alex Mkama alisema tukio la kwanza limetokea Mei 26 mwaka huu katika kijiji cha Simbalambende kata ya Ruaha wilayani Kilosa.
Kamanda huyo alimtaja Said Kandulu (52) mkazi wa Simbalambende alifariki dunia baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali eneo la kifuani upande wa kushoto.
Alimtaja mtuhumiwa wa tukio hilo kuwa ni Lucas Zacharia Kanyenze (64) mkazi wa Hyamvisi ambapo alisema chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi .
"Marehemu alikuwa anamtuhumu mtuhumiwa kuwa kamuoa mtalaka wake ,ugomvi huo ulichochewa na ulevi"alisema.
Katika tukio la pili jeshi la polisi mkoani hapa linamshikilia Ayubu Rashid Ayubu (23) mkazi wa Gang'anda kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi .
Alisema tukio hilo limetokea Mei 29 mwaka huu majira ya Asubuhi katika kitongoji cha Gang'anda, kijiji cha Mfuru, kata ya Tegetero wilayani Morogoro.
Kamanda huyo alimtaja Rashid Ayubu Juma (71) mkazi wa Gang'anda alikufa kwa kushambuliwa na panga eneo la kichwani upande wa kisogoni na mwanae wakati marehemu akiwa amepumzika nyumbani kwake.
Alisema kijana huyo ghafla alianza kumshambulia kisogoni mithiri ya kukata mti na kusababisha kupoteza maisha na kwamba mtuhumiwa amekamatwa ambapo alisema chanzo cha tukio hilo ni matatizo ya Afya ya akili.
0 Comments