Header Ads Widget

WANAFUNZI VYUONI DODOMA WATOA MIKAKATI YA KUKABILIANA NA UHALIFU KWA USHIRIKIANO NA POLISI

 

  Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima App Dodoma

Wanafunzi wa vyuo vikuu mkoani Dodoma wameamua kuacha kuwa watazamaji wa vitendo vya uhalifu kwenye taasisi zao na badala yake wamechukua hatua—kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani humo, kuweka mikakati ya pamoja ya kuhakikisha usalama wao chuoni.

Katika kikao kilichowakutanisha na polisi mnamo Mei 15, 2025, viongozi wa serikali za wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali walijadili mbinu mpya za kupambana na changamoto kama ukatili wa kijinsia, wizi wa kimtandao, mahusiano hatarishi, na mitindo ya maisha inayohatarisha usalama wa wanafunzi.

Wakizungumza kwa niaba ya wenzao, baadhi ya viongozi walipendekeza kuanzishwa kwa klabu za uhamasishaji wa amani na maadili chuoni, kushirikiana na polisi katika kutoa elimu ya sheria kwa wanafunzi wapya, pamoja na kuanzisha vikundi vya ulinzi wa ndani vya kujitolea.


“Tunatambua hatuwezi kukaa kimya wakati uhalifu unatuathiri sisi moja kwa moja. Tunahitaji kuwa sehemu ya suluhisho,” alisema mmoja wa viongozi wa wanafunzi.


Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Katabazi, aliwapongeza wanafunzi kwa mwitikio wao na kuahidi kuwa jeshi hilo litakuwa tayari kushirikiana nao kwa karibu. Alieleza kuwa ulinzi shirikishi ni msingi wa usalama endelevu, na kwamba wanafunzi wakipewa nafasi, wanaweza kuwa chachu ya mabadiliko.

ASP Komeya Stephen alisisitiza umuhimu wa kuwajengea wanafunzi uwezo kupitia elimu ya usalama wa kidijitali, haki jinai na afya ya uzazi, akisema haya ni maeneo ambayo mara nyingi huzalisha migogoro na hatari chuoni.

Mbali na hayo, Mchungaji Rev. Ivo Livingstone Augustino kutoka St. John’s University aliwahimiza wanafunzi kuendeleza utamaduni wa kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale panapojitokeza viashiria vya uhalifu au migogoro.

Hatua hii mpya inawafanya wanafunzi wa vyuo mkoani Dodoma kuonekana si wahanga tu wa uhalifu, bali pia washirika muhimu katika kulinda amani na usalama ndani ya jamii ya elimu ya juu. 


 



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI