Header Ads Widget

WAKULIMA WAANZA KUONA TIJA YA BBT KWENYE ZAO LA PAMBA.

 

Bulugu Maige, (kushoto) ambaye ni mkulima wa Pamba kutoka Kijiji Ndoleleji wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga, akiwa na Wakulima wenzake wakifurahia mavuno ya zao la Pamba shambani baada ya uzalishaji kuongezeka.



Na COSTANTINE MATHIAS, Kishapu-Shinyanga.


WAKULIMA wa Pamba wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga wameipongeza serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kuleta Mkakati wa kuongeza tija ya uzalishaji kwenye zao la Pamba.


Itakumbukwa kuwa, Septemba 2024, Wizara ya Kilimo ilizindua Mkakati wa huo kwa kusambaza Maafisa Ugani vijijini kupitia Mpango wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) pamoja na kugawa Matrekta yatakayowalimia wakulima kwa bei nafuu.


Wakulima hao wameeleza hayo kwa nyakati tofauti walipotembelewwa na wanadishi wa Habari za Pamba mashambani kwao na kusisitiza kuwa tangu waanze kusimamiwa na Maafisa Ugani kwenye mashamba yao, kuna mabadiliko kwenye uzalishaji pia wamepata huduma za Ugani kwa wakati tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.


Jastine Bundala, mkulima wa Pamba kijiji cha Mhangu wilayani humo, anasema kwa miaka mitatu sasa, wamepata Elimu ya Kilimo bora kupitia kwa Maafisa Ugani wa BBT ambao wameletwa na serikali ili kuongeza tija ya zao la Pamba.


"Vijana hawa wamefanya mikutano mingi na kuelimisha namna ya kulima, kupanda, kupata mbegu bora na wametoa Elimu nzuri na Wakulima waliozingatia Elimu hiyo watapata mavuno mengi...nitarajia kuvuna zaidi ya kilo 800 kwa ekari moj tofauti na zamani tulikuwa tunapata kilo 200 mpaka 300 kwa ekari moj" anasema.


Mabungo Shija, mkulima wa Kijiji cha Mhangu wilayani humo anaipongeza serikali kwa kuajiri Maafisa Ugani kupitia Mpango wa BBT ambao wametoa Elimu ya Kilimo vha Pamba huku wakitarajia kupata mavuno mengi.


Anaiomba serikali kuongeza Maafisa Ugani ili wawafikie wakulima wengi zaidi huku akieleza kuwa kutokana na elimu waliyopatiwa wameona Mafanikio huku wakitarajia kupata mavuno mengi.


Naye Bulugu Maige, mkulima wa Kijiji cha Ndoleleji wilayani Kishapu anasema huko nyuma wakulima wa Pamba walikuwa hawana Elimu ya uvunaji sahihi na kwamba wanafauata maelekezo ili kupata Pamba yenye Ubora na inayohitajika kwenye soko la kimataifa.



Maige anawashauri wakulima wa pamba kufuata maagizo ya wataalamu wa kilimo ili kuvuna Pamba safi na yenye Ubora.


Mayunga Madaha mkulima wa Kijiji cha Ndoleleji, anasema Maafisa Ugani hao wamerejesha tabasamu ya uzalishaji wa Pamba kwa wakulima sababu wameanza kupata Pembejeo kwa wakati na uwiano sahihi.


"Ujio wa BBT umesaidia kupata takwimu za mashamba na wamesaidia Kugawa Pembejeo (dawa, pambu za kupulizia) kwa idadi na uwiano sawa...tunashukuru namna wanavyojituma asubuhi, mchana na jioni, na tunaomba serikali utuongezee Maafisa Ugani sababu tumeona matokeo yao" anasema Madaha.


Ofisa Kilimo kutoka Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) Edward Nyawile, anasema serikali kwa kushirikiana na Makampuni ya ununuzi wa Pamba, wamesambaza Maafisa Ugani zaidi ya 700 kupitia Mpango wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) ili kuhudumia wakulima wa Pamba katika mikoa inayolima zao la Pamba.


Usambazaji wa Maafisa Ugani kupitia Mpango wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT), wenye lengo la kuhudumia wakulima wa pamba, ni moja ya Mkakati wa Wizara ya Kilimo  ili kuhakikisha sekta ya Pamba inaongeza uzalishaji na Wakulima wanapata tija.


Mwisho.


Mayunga Madaha mkulima wa Kijiji cha Ndoleleji, akiongea na waandishi wa Habari, namna alivyonufaika na Mpango wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) kwenye Kilimo cha Pamba.


Bulugu Maige, mkulima wa Pamba kijiji cha Mhangu wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga akivuna Pamba shambani kwake, huku akitarajia kupata mavuno mengi kutokana na elimu aliyopewa na Maafisa Ugani wa BBT.



Wakulima wa pamba kijiiji cha Ndoleleji wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga wakivuna Pamba shambani.


Mayunga Madaha mkulima wa Kijiji cha Ndoleleji, akiongea na waandishi wa Habari (hawapo pichani) namna walivyonufaika na Mpango wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT).









Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI