NA MATUKIO DAIMA MEDIA
Mamia ya wakazi wa Iringa Mjini na vijijini, viongozi wa chama na serikali, pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo, walikusanyika katika kijiji cha Kiwele kushiriki mazishi ya aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kiwele wilaya ya Iringa vijijini marehemu Felix Waya huku wakili Sosten Mbedule akisema kifo chake kimegusa wengi.
Mazishi hayo yalifanyika katika kijijini kwake Mgela huku huzuni kubwa zikitawala wakati wa hotuba mbali mbali za viongozi na waombolezaji .
Miongoni mwa walioguswa na kifo hicho ni Wakili maarufu Sosten Mbedule, ambaye alimuelezea marehemu Felix Waya kama kiongozi wa mfano, mchapakazi na aliyekuwa na maono ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.
Akizungumza na Matukio Daima Media mara baada ya mazishi hayo, Mbedule alisema kuwa kifo cha Waya si pigo tu kwa familia yake, bali pia ni pengo kubwa kwa jamii ya Iringa na chama chake cha Mapinduzi (CCM) alichokitumikia kwa moyo mmoja.
“Kifo cha Diwani Waya kimetugusa wengi. Huyu alikuwa kiongozi mwenye maono, msikivu na aliyetumia muda wake mwingi kuwahudumia wananchi bila kuchoka. Alikuwa chachu ya maendeleo, mtu wa vitendo kuliko maneno,” alisema Wakili Mbedule kwa huzuni.
Diwani Felix Waya alifariki dunia ghafla juzi, muda mfupi baada ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa wananchi wa kata yake.
Tukio hilo lilifanyika wakati wa ziara rasmi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin, ambaye alikuwa akifanya ukaguzi wa shughuli za chama na serikali katika kata ya Kiwele.
Inaripotiwa kuwa mara baada ya kuwasilisha taarifa hiyo, Waya alipata mshituko na kuanguka, na juhudi za kumuokoa ziligonga mwamba.
Wananchi waliohudhuria mazishi hayo walielezea kwa masikitiko jinsi walivyompenda kiongozi huyo kutokana na uadilifu wake, uhusiano wake mzuri na wananchi, pamoja na juhudi zake za kuboresha huduma za kijamii kama vile elimu, afya, maji na miundombinu.
“Diwani wetu alikuwa karibu sana na wananchi hakutegemea vikao vya ofisi pekee, bali alikuwa mtu wa kushuka chini na kusikiliza matatizo ya watu alikuwa anatusaidia hata kwa fedha zake binafsi pale alipoona hakuna msaada wa haraka,” alisema Bi. Rehema Komba, mkazi wa Kiwele.
Viongozi wa chama na serikali waliotoa salamu zao wakati wa mazishi walimwelezea marehemu kama askari wa mstari wa mbele katika mapambano ya kimaendeleo.
Walisema kuwa Waya alikuwa mmoja wa madiwani waliokuwa wakitekeleza kwa vitendo Ilani ya chama na kujali ustawi wa wananchi kuliko maslahi binafsi.
Mazishi hayo yalihudhuriwa pia na viongozi wa dini mbalimbali, mashirika ya kiraia, wawakilishi wa halmashauri ya Iringa Vijijini na wananchi kutoka kata jirani waliokuja kutoa heshima zao za mwisho.
0 Comments