Kwenye misa maalumu ya misa iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro kabla ya kuanza kwa uchaguzi wa Papa mpya, Dekano wa Makardinali, Kardinali Giovanni Battista Re, amewaasa makardinali wapiga kura kuweka mbele masilahi ya Kanisa na ubinadamu badala ya misimamo binafsi.
Akihubiri leo asubuhi Jumatano, Mei 7, 2025 mbele ya maelfu ya waumini na viongozi wa Kanisa Katoliki waliokusanyika kwa sala na tafakari, Kardinali Re aliainisha kuwa kiongozi huyo mpya wa Kanisa atakayechaguliwa ni lazima aongozwe na amri kuu ya upendo.
"Papa ajaye anapaswa kuwa kiongozi anayewatumikia wote kwa moyo wa upendo, unyenyekevu na hekima ya kiroho. Ni lazima awe tayari kubeba mzigo wa majukumu makubwa ya kiroho na kijamii kwa ajili ya Kanisa zima na dunia," amesema Kardinali Re.
Aliwataka makardinali wapiga kura kuhakikisha kuwa mchakato wa kumchagua Papa mpya unaendeshwa kwa kutanguliza uaminifu kwa mafundisho ya Kanisa na uongozi wa Roho Mtakatifu.
"Tunapaswa kuepuka kushawishika na mitazamo ya kibinafsi au makundi, bali tuangalie kwa mapana mustakabali wa Kanisa na ustawi wa wanadamu wote," aliongeza.
MWISHO.
0 Comments