Na Moses Ng’wat, Mbozi.
Chama cha United Democratic Party (UDP) Mkoa wa Songwe kimetangaza msimamo wake wa kumuunga mkono mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 17, 2025, na Katibu wa UDP mkoani humo, Daud Myombe, wakati wa ibada maalum ya dua ya kumuombea Rais Dkt. Samia na viongozi wengine wa kitaifa, uchaguzi mkuu na kudumisha amani, iliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Vwawa, wilayani Mbozi na kuandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Songwe.
Myombe amesema chama chake kwenye nafasi ya urais watampigia kura mgombea wa CCM Dkt. Samia ambaye tayari amepitishwa na chama chake.
Amesema wameamua kwa hiari kumuunga mkono Dkt. Samia kutokana na kazi nzuri anayoifanya ya kuliletea taifa maendeleo.
Hata hivyo akawaomba wananchi wawapatie nafasi wagombea wa UDP katika watakaosimamishwa na chama hicho kwenye nafasi za ubunge na udiwani ili chama hicho kipate fursa ya kuchangia maendeleo ya nchi kupitia uwakilishi bungeni na kwenye halmashauri.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma) Mkoa wa Songwe, Nikubuka Kayuni, alipongeza serikali ya mkoa kwa kuendelea kuweka mazingira ya haki kwa vyama vyote vya siasa kufanya shughuli zao kwa amani.
Pia alitoa rai kwa viongozi wa dini kutumia majukwaa yao kutoa ushauri wa kujenga kwa viongozi wa kisiasa kabla mambo hayajaharibika.
Katika shughuli hiyo ya dua, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (MNEC) Mkoa wa Songwe, Aden Mwakyonde, aliyemwakilisha Mwenyekiti wa CCM Mkoa, aliwaasa wananchi kudumisha amani akieleza kuwa baadhi ya nchi za Afrika zilizopuuzia amani zimejikuta katika machafuko yasiyokoma.
“Ni jukumu la kila Mtanzania kuilinda amani na tunapaswa kujifunza kwa mataifa yaliyovurugika, hivyo nafasi hii ninawapongeza Waislamu wa Songwe kupitia BAKWATA kwa kuandaa tukio hili la dua maalum lenye nia ya kuunganisha taifa,” alisema Mwakyonde.
Kwa upande mwingine, Chifu wa Himaya ya Wanyiha, Sibhelwa Nzunda, aliwataka wazazi kuwaelimisha watoto kuhusu thamani ya amani na kukemea siasa za chuki, akionya pia dhidi ya matukio ya mauaji ya albino na utekaji nyara katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.
Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Hussein Batuza, alisema dua hiyo imelenga kuiombea nchi amani, haki na utulivu wakati wa uchaguzi na kuwataka Watanzania kuwa wazalendo na kukataa kuchochewa kuvuruga amani.
“Watanzania tuilinde amani yetu na tuwakatae watu au viongozi wenye nia ya kuchochea uvunjifu wa amani kwa misingi ya dini au siasa na viongozi wa dini mna wajibu wa kuishauri serikali kwa hekima na maadili badala ya kuiamrisha,” alisisitiza Shekhe Batuza.
Akihitimisha, Mkuu wa Wilaya ya Momba, Elias Mwandobo, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, alisisitiza kuwa jukumu la kudumisha amani ni la kila mtu na madhehebu yote, huku Akiwaasa viongozi wa dini kuendelea kuhubiri maadili, mshikamano na uzalendo kwa taifa.
Mwisho.
0 Comments