Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kutishiwa maisha kwa Ndugu Boniphace A. K. Mwabukusi, Wakili Mwandamizi, Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la TLS.
Tarehe 10 Mei 2025, Wakili Mwabukusi alipokea ujumbe wa vitisho kupitia namba ya simu ya Tanzania (0792705831), ujumbe uliodai kuwepo kwa njama ovu za kuondoa uhai wake.
TLS inalaani vikali tukio hilo na kulikemea kwa nguvu zote, kwani ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na sheria nyingine za nchi.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 4(d) cha Sheria ya TLS, Sura Na. 307 ya Sheria za Tanzania, TLS ina jukumu la kulinda wanachama wake na umma kwa ujumla, hivyo inachukulia kwa uzito mkubwa suala hili.
Kila Mtanzania ana haki ya kuishi na kufanya kazi zake halali kwa amani na bila hofu, wakiwemo wanasheria kama Wakili Boniphace A. K. Mwabukusi.
TLS inatoa wito kwa vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi, kufanya uchunguzi wa kina, kuwatambua na kuwachukulia hatua za kisheria wote waliohusika na vitisho hivyo.
Kwa kuwa vitisho hivi vinahusiana moja kwa moja na nafasi ya Wakili Mwabukusi kama Rais wa TLS na msemaji wa taasisi, TLS itafuatilia kwa karibu mwenendo wa uchunguzi huu na kuchukua hatua stahiki za kisheria ikiwemo mashauri ya kimkakati mahakamani (strategic litigations) endapo itahitajika.
Tukio hili ni tishio si tu kwa Wakili Mwabukusi, bali kwa taasisi nzima ya TLS. Hatuwezi kukaa kimya huku kiongozi wetu mkuu akitishiwa maisha kwa kutimiza wajibu wake wa kisheria na kitaaluma. Uhalifu huu ni wa kulaumiwa na hauwezi kuvumiliwa kamwe.
TLS itaendelea kutimiza majukumu yake ya msingi kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni pamoja na kusimamia haki, usawa na utawala wa sheria. Ifahamike kuwa hakuna aliye juu ya sheria.
Imetolewa na:
Baraza la Uongozi la Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS)
Wakili Laetitia Petro Ntagazwa
Makamu Rais – TLS
0 Comments