kioo cha gari kilichovunjwa kwa mawe
NA MATUKIO DAIMA MEDIA ,IRINGA
Taharuki imetanda kwa watumiaji wa barabara ya Iringa–Dodoma, hasa katika eneo la Mlima Nyang’oro, kufuatia matukio ya magari kurushiwa mawe na kuvunjwa vioo na watu wasiojulikana, hali inayohatarisha usalama wa abiria na kusababisha uharibifu wa mali.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa madereva wanaotumia barabara hiyo, matukio hayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara hasa nyakati za usiku na mapema asubuhi.
Baadhi ya magari yameripotiwa kuvunjwa vioo na kuharibika sehemu mbalimbali kutokana na kurushiwa mawe.
Obadia Mduda, mmoja wa madereva wanaotumia barabara hiyo, ameeleza kuwa tukio hilo lilimkumba usiku wa tarehe 3 mwezi huu akiwa safarini kuelekea Dodoma.
“Nilipokuwa napita eneo hilo usiku, ghafla kitu kizito kilitua ndani ya gari langu.
Baada ya kuangalia, niligundua ni jiwe lililopasua kioo cha mbele cha gari.
Tuliingiwa na hofu kubwa, ila kwa bahati nzuri tuliweza kuondoka kwa haraka na kutoa taarifa kituo cha polisi cha karibu.
Hata hivyo, hatukuona hatua yoyote ya haraka ikichukuliwa,” alisema Mduda.
Musa Nyembo, dereva wa lori la makaa ya mawe kutoka Kenya, alielezea hofu yake akisema
“Vitendo hivi vinatisha sana, hasa kwetu madereva.
Usalama wetu unakuwa mashakani kila tunapopita eneo hili. Naiomba serikali, hasa Jeshi la Polisi, kuimarisha ulinzi katika eneo hili na kuwachukulia hatua wahusika.”
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi, hazikufanikiwa. Hata hivyo, Matukio Daima TV ilizungumza na Katibu Tarafa wa Isimani, Thomas Myinga, ambaye alithibitisha kuwa Jeshi la Polisi tayari linawashikilia watu watatu wanaodaiwa kuhusika na matukio hayo.
Myinga alisema uchunguzi bado unaendelea ili kubaini sababu na nia ya wahusika waliokamatwa, na kusisitiza kuwa vyombo vya usalama vimejipanga kuhakikisha wote waliohusika wanachukuliwa hatua stahiki mara baada ya uchunguzi kukamilika.
0 Comments