Na Matukio Daima Media
TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) kwa kushirikiana na Agha Khan Foundation, Tanzania leo Mei 20, 2025 wamepanda miti zaidi ya 200 katika zoezi la kulinda mazingira kwa kuanzisha msitu bustani.
Zoezi hilo ni katika kuelekea Maadhimisho ya Miaka 50 ya TET yanayotarajia kufanyika Juni mwaka huu, limefanyika katika Makao Makuu ya TET, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk. Aneth Komba ameishukuru Agha Khan Foundation kwa hatua hiyo kwani wanatekeleza kwa vitendo utunzaji wa mazingira na kulinda mabadiliko ya tabianchi.
"TET katika kusheherekea miaka 50 inaendeleza utunzaji wa mazingira kwa vitendo kwani hata katika maboresho ya mitaala ya kielimu tumezingatia utunzaji mazingira.
"Maboresho ya mitaala ya mwaka 2023 yameweka somo la jiografia kuwa ni somo la lazima na katika somo hilo tumewezesha wanafunzi kuhimili na kutunza mazingira," amesema.
Nae Mkuu wa Programu wa Agha Khan Foundation Tanzania, Carolyn Mlewa amesema wamepanda miti hiyo zaidi ya 200 yenye aina 25 tofauti ikiwemo ya kivuli, matunda, dawa, na miti pori kama ishara ya kulinda mazingira.
Msimamizi wa Mradi wa Mazingira wa taasisi hiyo, Japhet Wangwe amesema amesema upandaji msitu huo mdogo ni moja ya hatua ya kuboresha mazingira lakini pia kuhifadhi viumbe vya asili na vya kiikolojia.
0 Comments