Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima APP Dodoma
SEKTA ya sheria nchini Tanzania imeingia katika zama mpya za mageuzi ya kidijitali, baada ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuweka msukumo mkubwa katika matumizi ya TEHAMA kwa ajili ya kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa haki.
Akizungumza jijini Dodoma leo Mei 20, 2025, wakati akieleza mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita ambapo Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, alisema kuwa hadi kufikia Aprili mwaka huu, asilimia 75 ya mifumo ya TEHAMA inayotoa huduma za kisheria nchini imeunganishwa, hatua inayowezesha taasisi mbalimbali za sheria kushirikiana kwa karibu na kwa wakati halisi."
Serikali imejipanga kuhakikisha huduma za kisheria zinapatikana kwa haraka, kwa gharama nafuu na kwa njia inayomjali mwananchi wa kawaida TEHAMA ndiyo daraja la kufanikisha hilo," alisema Dkt. Ndumbaro.
Waziri huyo alibainisha kuwa matumizi ya mfumo wa Portal ya HAKI SHERIA yamesaidia wananchi kuwasiliana moja kwa moja na maafisa wa msaada wa kisheria waliopo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 184, huku mfumo wa e-CMS ukibadilisha namna mashauri yanavyosajiliwa, kupangwa na kusikilizwa kwa njia ya mtandao, hivyo kupunguza ucheleweshaji wa haki.
Aidha, mfumo wa TTS (Transcription and Translation System) umeongeza kasi ya kutafsiri hukumu na kumbukumbu za mashauri kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza kwa muda mfupi—dakika chache tu—ikilinganishwa na siku au wiki kwa mfumo wa kawaida.
Katika kuimarisha utoaji wa huduma za kisheria kwa wananchi vijijini na mijini, huduma za usajili wa vizazi, vifo, ndoa, talaka na udhamini sasa zinapatikana kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa eRITA, unaomwezesha mwananchi kutuma maombi na kuchukua nyaraka kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya bila kuhangaika.
Waziri Ndumbaro aliongeza kuwa Serikali pia imeongeza idadi ya Ofisi za Mashtaka za Wilaya kutoka 53 mwaka 2021 hadi 108 mwaka 2025, huku idadi ya watoa huduma wa utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala ikifikia 498, hatua inayolenga kupunguza msongamano wa kesi mahakamani.
Kwa upande wa elimu ya sheria, Dkt. Ndumbaro alisema kuwa wataalamu 2,375 wa sheria wamehitimu kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo tangu 2021, huku wanafunzi 2,876 wakihitimu katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto, hatua inayopanua wigo wa upatikanaji wa huduma za kisheria nchini.
Katika kuthibitisha viwango vya kitaifa katika kulinda haki za binadamu, Waziri alieleza kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imepata Daraja A kutoka GANHRI – kiwango cha juu kinachotambua taasisi zinazotekeleza majukumu yao kwa viwango vya kimataifa.
"Tanzania inasimama imara kama mfano wa nchi zinazoendeleza haki, sheria na utawala bora kwa njia shirikishi na ya kidijitali," alisema Dkt. Ndumbaro.
Mwisho
0 Comments