Header Ads Widget

SERIKALI YAFANYA UWEKEZAJI MKUBWA SEKTA YA UVUVI ZIWA TANGANYIKA

Na Fadhili Abdallah,Kigoma 

Serikali kupitia wizara ya mifugo na uvuvi imekabidhi  boti 19 zenye thamani ya shilingi bilioni 1.1 za uvuvi na doria kwa ajili ya kuimarisha uvuvi kwenye mwambao wa ziwa Tanganyika mkoani Kigoma.

Naibu Katibu Mkuu wizara ya mifugo na uvuvi, Dk.Edwin Mhede alikabidhi boti hizo katika Mwalo wa katonga Manispaa ya Kigoma Ujiji  mkoani Kigoma ikiwa ni sehemu ya mpango wa serikali kuhakikisha shughuli za uvuvi zinakuwa na tija kubwa nchini.

Katika boti zilizokabidhiwa zipo boti 11 kwa ajili ya kufanya doria kwenye mwambao wa ziwa Tanganyika zenye thamani ya shilingi milioni 539 ambazo zimekabidhiwa kwa vikundi vya ulinzi wa rasilimali za uvuvi ziwa Tanganyika (MBU’s) Sambamba na boti nane za kisasa za uvuvi  zenye thamani ya shilingi milioni 607.3 .

Naibu Katibu Mkuu huyo  pamoja na boti amekabidhi pia vifaa vya kuvulia ikiwemo kifaa cha kuangalia wingi wa samaki (Fish Finder), nyavu, maboya na vifaa muhimu za kusaidia uvuvi wa kisasa wenye tija.

Akizungumza kabla ya kukabidhi boti hizo Naibu Katibu Mkuu wizara ya mifugo na uvuvi,Dk.Edwin Mhede alisema kuwa serikali imedhamiria kuona shughuli za uvuvi zinafanyika kisasa ili kuwezesha kupata uzalishaji mkubwa wa mazao ya uvuvi na kuimarisha uchumi wa wavuvi na kuongeza mapato ya serikali.

Awali Mkurugenzi wa uvuvi kutoka wizara ya mifugo na uvuvi, Profesa Mohamed Sheikh  alisema kuwa kwa mwaka wa fedha  2024/2025 Rais Samia ametoa kiasi cha shilingi Bilioni 11.5 kwa ajili ya ununuzi wa boti za kisasa 120 za uvuvi na doria  nchini na vifaa vya kisasa vya uvuvi ambapo kati ya hizo  ziwa Tanganyika limepatiwa  boti 19 ambazo tayari zimetolewa. 

Profesa Sheikh alisema kuwa boti hizo zitawezesha wavuvi kwenda kwenye maji ya kina kirefu kwa ajili ya kuvua hivyo kuondokana na tabia ya kuvua pembezoni mwa ziwa ambako kuna mazalia ya samaki sambamba na  boti za doria ili kuzuia uvuvi kwenye maeneo tengefu kwa ajili ya mazalia ya samaki.


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI