Mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi amepokea tuzo 2 za utoaji huduma bora za afya Ä·itaifa kwa manispaa ya Musoma.
Tuzo hizo zimetolewa hivi karibuni na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na TAMISEMI kwa manispaa hiyo kuoitia kituo cha afya Nyasho na zahanati ya Kwangwa kwa kufanya vizuri kitaifa.
Akipokea tuzo hizo hii leo mei 15,2025 kutoka kwa viongozi wa bituo hivyo na wataalam wa afya amesema tuzo hizo zimeutangaza vyema mkoa wa Mara kitaifa kwa kufanya mambo mazuri.
Kanali Mtambi amewapongeza viongozi wa vituo hivyo na wasimamizi wa huduma za afya manuspaa ya Musoma na mkoa wa Mara kwa kazi nzuri.
Amesema vituo hivyo kushinda kufuatia tathmini iliyofanywa na wataalamu wa afya hapa nchini sio jambo dogo na pongezi zinastahili kutolewa.
“Kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Mara ninakipongeza Kituo cha Afya Nyasho na Zahanati ya Kwangwa kwa utoaji wa huduma nzuri kwa wananchi na kwa ushindi walioupata kitaifa ambao umetuletea heshima katika mkoa wetu”
" Inafurahisha kuona mkoa wa Mara ukitajwa katika mambo mazuri yanayoonyesha uhodari na utendaji kazi wa watumishi wa mkoa wa Mara katika kuwatumikia wananchi",amesema.
Kufuatia ushindi wa tuzo hizo mkuu huyo wa mkoa ametoa shilingi milioni 1 kwa kila kituo kama motisha na kuiagiza Wilaya na Manispaa ya Musoma pia kutoa fedha kwa ajili ya kuwapa motisha watumishi waliofanikisha upatikanaji wa tuzo katika vituo hivyo.
Aidha Kanali Mtambi ameishukuru Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI) kwa kuandaa tuzo hizo ambazo zinatabua juhudi kubwa zinazofanywa na wataalamu katika maeneo mbalimbali kuokoa maisha ya watanzania.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka amewapongeza watumishi na uongozi wa vituo hivyo kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuahidi kushirikiana na Mkurugenzi wa Manispaa kutoa shilingi 1,500,000 kwa kila kituo ili kuunga mkono maono ya mkuu wa mkoa ya kuwapongeza watumishi hao.
“Hizi ni tuzo za utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kama Wilaya tunashukuru sana vituo vyetu viwili kupata ushindi huu kimkoa na Kitaifa jambo linaloonyesha huduma zetu ni nzuri",amesema.
Amesema Kituo cha Afya Nyasho kimekuwa mshindi wa kwanza kati ya vituo vya afya zaidi ya 3,700 vinavyotoa huduma za afya hapa nchini huku Zahanati ya Kwangwa ikiwa miungoni mwa zahanati 17 nchini zilizofanya vizuri katika utoaji wa huduma.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa mkoa wa Mara Dk.Zabron Masatu amesema vituo vya kutolea huduma vilifanyiwa tathmini nchi nzima na matokeo yake Kituo cha Afya Nyasho kimekuwa mshindi wa kwanza kitaifa kati ya vituo vyote vya afya vilivyopo huku Zahanati ya Kwangwa ikiwa miungoni mwa zahanati 17 kitaifa zilizofanya vizuri.
Dk. Masatu amesema vigezo vya tuzo hizo vilikuwa ni pamoja na usafi wa vituo, ubora wa huduma, upatikanaji wa dawa, utunzaji wa takwimu na taarifa za afya, upatikanaji wa huduma kwa wakati na kadhalika.
0 Comments