Header Ads Widget

RED CROSS IMETOA AJIRA KWA WANANCHI 445 NCHINI - DKT BITEKO.

 



Na  Matukio Daima Media ,Dodoma

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema Serikali inaunga mkono mengi yanayofanywa na Chama cha Msalaba Mwekundu nchini kwani chama hicho hadi sasa kimefanikiwa kutoa ajira kwa wananchi zaidi ya 445 pamoja na vijana wa kujitolea 300,000.

Dkt Biteko alisema kuwa pamoja na hayo chama hicho kina matawi na matawi madogo zaidi ya 700 kila kona ya nchi na hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa watanzania na wahitaji wengine.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Mei 10, 2025 katika hotuba yake kwenye hafla ya maadhimisho ya miaka 63 ya chama hicho yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

"Mmeajili zaidi ya wafanyakazi 445 pamoja na vijana wa kujitolea 300000 nchi nzima na hivyo kufanya watanzania kuwa na moyo wa kujitolea kwenye nchi yao na kuwafanya kujua kuwahudumia watu wengine ni jambo la wajibu na kwamba huitaji kulipwa kumsaidia mtu".

"Mmetoa msaada wa hali na mali katika kipindi cha mafuriko kilichotokea Hanang Kateshi desemba 3,2023 ambapo chama chenu mlijenga nyumba 35 kati ya nyumba 101 zilizopangwa kujengwa na serikali sawa na asilimia 35  ya mahitaji yote ya nyumba"aliongeza 

Dkt Biteko alieleza kuwa ushiriki wa msalaba mwekundu katika kampeni ya kukusanya damu kwa kushirikiana na mpango wa damu salama nchini tangu mwaka 1949 hadi sasa, ujenzi wa kituo cha kukusanyia damu katika hospitali ya Wilaya ya kasulu mwaka 2017, damu waliyoikusanya kupitia kampeni zao imeokoa maisha ya watu wengi ambao pengine wangekosa uhai wao na matokeo yake wangezalisha wajane/wagane ama watoto yatima, ni kwa juhudi zao wameokoa maisha ya watu hao.

"Mmeshiriki katika shughuli zingine mbalimbali ikiwemo kutoa mafunzo ya huduma ya kwanza kwa watu binafsi, makampuni, mashirika na viwanda wakati wa janga la uviko 19 ninyi mlikuwa msitali wa mbele wakati wengine wanawakimbia watu ninyi mlirisk maisha yenu kuwasogelea wagonjwa na kuwahudumia, mliokoa maisha ya watu wengi mlifanya nchi yetu ibaki salama hata nisipoambiwa niseme lolote juu yenu hili nalo litoshe kusema msalaba mwekundu mmefanya kazi kubwa na mungu awabariki sana"alisema Biteko

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (Red Cross Society), David Kihenzile amesema mfumo wa uokoaji yaani huduma ya kwanza nchini bado haujaimarika kwa sababu inapotokea ajali au janga, wananchi wengi wanaokwenda kutoa msaada huwa hawana uwezo na maarifa yakutosha ya namna ya kutoa huduma hiyo.

Amesema katika watu kumi wanaopata ajali, watatu ndio hupata bahati ya huduma ya kwanza ambapo karibu asilimia 70 ya watu wanaofariki baada ya ajali ni kwa sababu hukosa huduma ya kwanza.

"Leo majumbani mwetu, kwenye magari yetu, kwenye vyombo vya umma, shule na taasisi, inapotokea changamoto, mfumo wetu wa uokoaji bado upo chini sababu wengi hawana uwezo wala maarifa mazuri ya namna ya kutoa huduma ya kwanza" ameongeza Kihenzile.


Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania, Lucia Pande amesema zipo changamoto wanazokabiliwa nazo ikiwemo muingiliano wa majukumu wakati wa utoaji wa huduma ya kwanza kwa waathirika wa majanga au ajali.

Amesema kwa upande wa nchi zingine chama kama hicho ndio wahusika wa kwanza wenye jukumu la kutoa huduma ya kwanza pale linapotokea janga, tofauti na hapa nchini kumekuwepo na mwingiliano mkubwa hasa kwa wasimamizi wa hiyo taasisi ambayo hupelekea kupunguza ufanisi wa shughuli zao.

Lucia ameiomba Serikali kusaidia kuweka utofauti wa majukumu na kukipa kipaumbele chama hicho kwa kukiongezea bajeti ambayo imekuwa ikipungua kila mwaka.

"Tunatamani Serikali isaidie wale ambao wanasimamia wafanye usimamizi tu, wasiingie kwenye kutoa huduma ili sisi tunaotoa huduma tubaki na jukumu la kutoa huduma, hiki pia mgeni rasmi ni chanzo cha mapato kwa hiyo, ili mikoa yetu iweze kuwa 'active' ni lazima itoe hizi huduma kwa kulipia, tunaita Comercial First Aid" amesema Lucia.

MWISHO.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI