Header Ads Widget

TANZANIA YAJIKITA KUIMARISHA VIWANDA NA UZALISHAJI KWA MSOKO YA NDANI KITAIFA

 


   Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima App Dodoma

SERIKALI ya Tanzania imeimarisha juhudi za kuendeleza viwanda na kuongeza tija ya uzalishaji wa bidhaa zinazolenga masoko ya ndani na nje ya nchi, ikiwa ni sehemu ya ajenda ya maendeleo ya uchumi wa viwanda iliyoasisiwa na Serikali ya Awamu ya Sita.

Akizungumza jijini Dodoma, Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo alisema kuwa Tanzania imeendelea kujitanua katika masoko ya kimataifa, sambamba na kuwekeza katika miundombinu ya viwanda, uboreshaji wa ubora wa bidhaa na kuwajengea uwezo wajasiriamali.


“Mwelekeo wetu si tu kuuza zaidi nje ya nchi, bali kuhakikisha tunazalisha kwa ubora unaokubalika kimataifa na kukuza ajira kupitia viwanda vya ndani,” alisema Dkt. Jafo.

Kwa mujibu wa Waziri, kati ya mafanikio makubwa ni ongezeko la mauzo ya bidhaa katika soko la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutoka dola milioni 1,303.4 mwaka 2021 hadi dola milioni 2,968 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 127.7. Mauzo ya bidhaa barani Afrika kwa ujumla yaliongezeka kwa asilimia 61.2 katika kipindi hicho.

Aidha, Tanzania imenufaika na mpango wa AGOA unaoiwezesha nchi kuuza bidhaa kwa Marekani bila ushuru, ambapo mauzo yaliongezeka kwa zaidi ya asilimia 150 ndani ya miaka mitatu. Pia, mauzo kwenda Umoja wa Ulaya yaliongezeka kwa asilimia 38.5.

Katika kuimarisha ubora wa bidhaa, TBS imetoa leseni 2,569 za nembo ya ubora na kufanya ukaguzi wa bidhaa zaidi ya laki tatu, huku BRELA ikisajili makampuni, alama za biashara na leseni za viwanda kwa kasi kubwa.

Kwa upande wa viwanda, Dkt. Jafo alieleza kuwa Tanzania sasa ina viwanda 14 vya saruji na 36 vya mbolea, ambapo baadhi vina uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 800,000 kwa mwaka. Aidha, uzalishaji wa saruji umeongezeka zaidi ya mara mbili tangu mwaka 2019.


Sekta ya kilimo pia imenufaika kupitia mfumo wa stakabadhi za ghala, ambapo tani zaidi ya 654,000 za mazao zimeuzwa kwa wakulima, na kuingiza shilingi trilioni 4.9 na kuunda ajira karibu 7,000.

Katika juhudi za kuendeleza mazingira ya biashara, jumla ya masoko 367 yamejengwa na kuboreshwa nchi nzima, na kuwawezesha zaidi ya wafanyabiashara 136,000 kufanya kazi katika mazingira bora.

Dkt. Jafo alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuwekeza katika ujenzi wa viwanda, uboreshaji wa bidhaa na kusaidia wajasiriamali wadogo na wa kati kupitia mikopo na mafunzo, ili kukuza uchumi wa viwanda unaojitegemea na ushindani wa kimataifa.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI