Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi akizungumza mara baada ya zoezi la usafi kumalizika
Katibu tawala Mkoa wa Mwanza Elikana Baladya wa pili kushoto wakishirikiana na Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi kufanya usafi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya mazingira duniani
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA
Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayofanyika kila mwaka Juni 5, Wilaya ya Nyamagana, Mkoa wa Mwanza, imeadhimisha siku hiyo kwa kufanya usafi katika stendi ya daladala ya Buhongwa pamoja na soko la eneo hilo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutunza mazingira.
Akizungumza mara baada ya zoezi hilo la usafi, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, amesema kuwa usafi wa mazingira ni hatua muhimu katika kupunguza taka na kuzuia magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.
“Kitendo cha kufanya usafi leo ni kuendelea kuhamasisha na kuhimiza wananchi kutotumia mifuko ya plastiki iliyozuiliwa, ambayo huharibu mazingira ya Taifa letu,” alisema Makilagi.
Ameongeza kuwa kwa mwaka huu, Wilaya ya Nyamagana imelenga kupunguza taka ngumu na kuhimiza upandaji wa miti ili kupunguza hewa ya ukaa, sambamba na kushirikiana na wananchi kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwa ustawi wa taifa.
Kwa upande wake, Afisa Afya wa Jiji la Mwanza, Audiptiace Sabbo, pamoja na Afisa wa Usafi na Mazingira wa jiji hilo, wamesisitiza kuwa wananchi wana jukumu la moja kwa moja katika kuzuia magonjwa yatokanayo na uchafu kwa kudumisha usafi kuanzia ngazi ya mtaa hadi kata.
“Hivyo sasa ni muhimu kwa kila mwananchi kuhakikisha anazingatia usafi wa mazingira. Sheria za serikali za mitaa zinaruhusu hatua kuchukuliwa dhidi ya yeyote anayechafua mazingira,” alisisitiza Sabbo.
Vilevile, Mwajuma Hamad, mwanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Nyabulogoya, na Samwel Joseph, mkazi wa Buhongwa, wamepongeza ushirikiano kati ya wananchi na serikali katika suala la usafi. Wameitaka serikali na wadau wa mazingira kuendelea kutoa elimu kuhusu mabadiliko ya tabianchi na njia za kuhimili athari zake.
Maadhimisho haya yanakuja wakati ambapo dunia inakumbwa na changamoto nyingi za kimazingira, na hatua kama hizi za kijamii zinachangia kwa kiasi kikubwa katika kulinda afya ya jamii na mazingira kwa ujumla.
0 Comments