Header Ads Widget

MPANJU AELEZA MAFANIKIO MPANGO WA KUTOKOMEZA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO

 

Na Hamida Ramdhan,Matukio Daima App Dodoma

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju, ameendelea kusisitiza umuhimu wa utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto, akieleza kuwa mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya ushirikiano wa pamoja kati ya Serikali, wadau wa maendeleo na jamii kwa ujumla.

Akionge leo Mei 29,2025 Katika kikao cha kujadili usawa wa kijinsia Mpanju alisisitiza kuwa, Matakwa ya kikatiba kuhusu usawa wa kijinsia lazima yatafsiriwe katika nyanja zote za maisha, kuanzia kwenye elimu, ajira, uongozi hadi katika mfumo wa sheria.

Ameongeza kuwa, licha ya kuwepo kwa sheria zinazolinda haki za wanawake, changamoto bado zipo katika utekelezaji wake, na mifumo mingi bado haijazingatia usawa huo. Hii ndiyo sababu Serikali na wadau wamekuwa wakitunga miongozo ya kisera inayolenga kuakisi maendeleo ya wanawake na watoto.

Kwa mujibu wa Mpanju, elimishaji kupitia programu hizi unalenga kuondoa mitazamo ya mfumo dume na kuwajengea wanawake uwezo wa kujitambua na kujitetea dhidi ya ukatili. Amesema kupitia juhudi hizo, Serikali imeanzisha madawati ya kijinsia shuleni kwa lengo la kuhimiza usawa kuanzia ngazi ya elimu ya msingi.


Alex Shayo, Mtakwimu kutoka Wizara hiyo na Mratibu wa Programu ya Kuwezesha Wanawake Kushiriki kwenye Masuala ya Uongozi na Usawa wa Kijinsia, amesema kuwa mafanikio makubwa yameanza kuonekana kutokana na ongezeko la uelewa miongoni mwa jamii. Amesema ripoti zinaonesha kuwa utoaji wa taarifa za ukatili umeongezeka, jambo linaloashiria kuwa wananchi sasa wana uelewa na ujasiri wa kuripoti matukio ya ukatili, hasa dhidi ya wanawake na watoto.

Kwa mujibu wa Shayo, takwimu zinaonesha kuwa tangu kuanzishwa kwa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto mwaka 2017, kiwango cha ukatili kilichokuwa asilimia 40 kimeshuka hadi kufikia asilimia 27 mwaka huu. Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto nyingi, ikiwemo miiko ya kimila na desturi ambazo zimeendelea kuendeleza mifumo dume inayowadhoofisha wanawake. Kwa kutambua hilo, Serikali imekuwa ikihusisha wadau mbalimbali ili kuhakikisha kila upande unahusishwa katika kuondoa mila kandamizi.

Mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Afisa Mradi kutoka taasisi isiyo ya kiserikali, alisema kuwa mpango huu unakwenda kugusa changamoto zote zinazowakabili wanawake, na kwamba mafanikio ya muda mrefu yanahitaji mshikamano wa jamii kwa ujumla.

Kwa upande mwingine, Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Lucy Uisso, amesema mafanikio katika uelewa wa haki za wanawake yanaonekana kupitia kesi zinazofikishwa mahakamani. Amesema, "Kwa sasa idadi ya wanaofikishwa mahakamani kwa makosa ya ukatili imeongezeka, huku wengi wao wakitiwa hatiani. Hii ni dalili njema kuwa haki inatendeka."

Kwa upande wake, Karina Dzialowska, Mkuu wa Idara ya Uchumi na Utawala Bora katika Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, amesema, "Tunajivunia kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa mpango huu wa mageuzi ya kijinsia. Tumetimiza miaka miwili ya utekelezaji na kikao hiki kimetupa nafasi ya kuonyesha mafanikio, changamoto na mipango ya baadaye.



Mpango huu unaoendeshwa kwa miaka saba umejikita katika maeneo muhimu kama vile kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi, kuboresha upatikanaji wa mikopo na huduma za kifedha kwa wanawake, kupambana na ukeketaji na ndoa za utotoni kupitia mashirika ya kiraia kama Pastoral Women’s Council (PWC) na Kanisa la Kilutheri Tanzania (ELCT), pamoja na kusaidia wanawake na wasichana kupitia mfuko wa TASAF.

Umoja wa Ulaya umetenga Euro milioni 90 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huu, ambapo Euro milioni 28 zinakwenda moja kwa moja katika bajeti ya Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuhakikisha masuala ya kijinsia yanazingatiwa katika mipango na bajeti zake. Msaada huo unatekelezwa kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wizara ya Afya, Wizara ya Katiba na Sheria (kupitia Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Mahakama), na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Zanzibar pia imenufaika kupitia bajeti maalum ya Euro milioni 7 inayoendeshwa kwa ushirikiano na UN Women.

Mpango huu unachangia moja kwa moja katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III 2021/22–2025/26) na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, ambazo zimeweka usawa wa kijinsia kama kipaumbele kikuu katika maendeleo ya taifa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI