Na Ashrack Matukio Daima App
Katibu mkuu wa wizara ya madini nchini Mheshimiwa Yahya Samamba ametoa rai kwa chama cha utoaji huduma za shughuli za madini (TAMISA) kuwa kupitia viongozi na wanachama wake kujiandaa kikamilifu kukabiliana na changamoto zozote za kiuchumi zitakazojitokeza katika sekta madini.
Mheshimiwa Samamba ametoa rai hiyo katika hafla ya uzinduzi wa bodi ya chama hicho (TAMISA) alipomwakilisha Waziri wa madini ,aliyetarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.
Aidha Mheshimiwa Samamba ameiasa bodi hiyo ya TAMISA kuhusu suala zima la ushirikiano kwa taasisi hiyo na wadau wengine katika sekta ya madini huku akiahidi kuwa Wizara ya madini itatoa ushirikiano kwa asilimia mia moja katika kuwezesha utekelezaji wa mambo yenye tija katika sekta hiyo.
Kuanzishwa kwa kamati hiyo ni sehemu ya maboresho katika suala zima la kuhudumia watu katika sekta ya madini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama hicho, Ndugu Peter Andrew ameeleza kuwa chama hicho kimekuja kuwa suluhisho kwa wadau wazawa katika sekta ya madini kuhakikisha kuwa wanaunganisha nguvu zao kwa pamoja kukabiliana na kasi ya maendeleo katika sekta hiyo.
Ndugu Sebastian Ndege ambae ni mkuu wa kitengo cha masoko na mawasiliano katika chama hicho ameahidi kuwa wao kama viongozi pamoja na wanachama wao watasimamia uwajibikaji , weledi na uwazi katika kutekeleza majukumu yake.
Naye Kamishna wa Tume ya Madini, Bi Theresia Nubi, ameeleza kuwa mbali na uzoefu aliokuwa nao katika suala zima la maudhui ya ndani (Local Content), yuko tayari kushirikiana na chama hicho pamoja na wadau wengine katika sekta ya madini kuhakikisha malengo yote yaliyowekwa na wizara yanatimia. Alisisitiza kuwa kwa kufanya kazi kwa pamoja, kutaimarisha si tu utekelezaji wa sera, bali pia kuinua uwezo wa wafanyabiashara wa ndani kunufaika na fursa zilizopo katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.
Aidha, Bi Nubi alitoa wito kwa taasisi mbalimbali kushiriki kikamilifu katika kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya umuhimu wa kushiriki katika mnyororo mzima wa thamani wa madini. Alieleza kuwa mafanikio ya sekta hayawezi kupatikana endapo kutakuwa na pengo kubwa la uelewa kati ya serikali, wawekezaji, na jamii zinazozunguka maeneo ya machimbo.
Mbali na hayo, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, Venance Kasiki, ameongeza kwa kusema kuwa ni wakati sahihi kwa wazawa kushirikiana kwa pamoja na TAMISA kuendana na kasi ya ukuaji wa soko la ndani. Alisisitiza kuwa hatua hiyo itawapa wazawa nafasi ya kutumia maarifa yao ndani ya mfumo rasmi wa biashara ya madini ili kufikia maendeleo jumuishi.
Alieleza kuwa ushirikiano huo utawezesha uanzishwaji wa miundombinu bora na huduma za kisasa zitakazowezesha madini kutoka kwa wachimbaji wadogo kufikia viwango vya kimataifa. Hii itaongeza ushindani wa bidhaa za ndani na kuleta tija katika sekta kwa ujumla, sambamba na kuongeza mapato kwa taifa na ajira kwa wananchi.
Hafla ya uzinduzi wa bodi ya chama hicho cha usambazaji wa huduma za madini(TAMISA) umefanyika leo hii Mei 16 ,2025 jijini Dar es salaam.
0 Comments